DCI waomba msamaha kwa Pasta waliyedhani ni mmoja wa watu waliovamia na kuchoma bunge

Idara hiyo ilibaini kwamba mchungaji huyo kwa jina Dennis Basweti hakuwa mmoja wa waliohusika katika uvamizi wa bungeni na waandamanaji, bali yeye alikuwa bungeni kwa mwaliko wa mbunge Silvanus Osoro.

Muhtasari

• "DCI imethibitisha kwamba maelezo ya Bw Dennis Basweti ni ya kweli, na imemfikia kwa kuomba msamaha, " chapisho la DCI lilisomeka kwa sehemu.

Silvanus Osoro akiwa bungeni na Pasta Dennis Basweti.
Silvanus Osoro akiwa bungeni na Pasta Dennis Basweti.

Siku moja baada ya idara ya uhalifu wa jinai, DCI kuchapisha makumi ya picha za kuwatambu washukiwa wa uhalifu uliofanyika bungeni na majengo mengine jijini Nairobi wiki jana wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha 2024, sasa idara hiyo imebaini kwamba ilifanya makosa katika kuchapisha baadhi ya nyuso za wahusika.

Kupitia ukurasa wao kwenye mtandao wa Facebook, DCI imebaini kwamba moja ya picha ambayo walichapisha ni ya mchungaji kutoka jimbo la Kisii ambaye alikuwa amealikwa bungeni na kiranja wa wengi katika bunge ambaye pia ni mbunge wa Mugirango ya Kusini, Silvanus Osoro.

Idara hiyo ilibaini kwamba mchungaji huyo kwa jina Dennis Basweti hakuwa mmoja wa waliohusika katika uvamizi wa bungeni na waandamanaji, bali yeye alikuwa bungeni kwa mwaliko wa Osoro, na hivyo kumuomba msamaha kwa kumharibia jina kwa umma kama mmoja wa wahalifu wanaotafutwa na mkono wa sheria.

Kwa chapisho lao, DCI walisema;

“Huku msako wa washukiwa wanaosakwa waliohusika na uhalifu wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa 2024 ukiendelea, DCI inataka kumwachia Bw Dennis Basweti ambaye picha yake iliorodheshwa miongoni mwa watu wanaosakwa.

Hii ni baada ya kutii wito wa DCI wa kuwataka watu walioorodheshwa kutembelea ofisi za DCI zilizo karibu ili kusaidia katika uchunguzi zaidi.

Mapema leo, Bw Basweti alijisalimisha katika afisi za DCI za Kenyenya na kurekodi taarifa iliyoonyesha kuwa picha zake zilizosambazwa akiwa amekalia bunge wakati wa maandamano zilipigwa mapema Juni 10, 2024, ambapo alitembelea kwa mwaliko wa Mbunge wake Mhe. Silvanus Osoro.

DCI imethibitisha kwamba maelezo ya Bw Dennis Basweti ni ya kweli, na imemfikia kwa kuomba msamaha, na kumpongeza zaidi kwa kuamini ahadi ya DCI ya kufanya uchunguzi kikamilifu na kwa haki.”

DCI walikuwa wamechapisha picha za nyuso za washukiwa Zaidi ya 20 ambao wanatuhumiwa kwa kuvamia bunge na kuharibu mali kabla ya kuteketeza sehemu ya jengo la bunge na wengine kuondoka na mali ya bunge wakati wa maandamano ya Gen Z Jumanne wiki iliyopita.