Charlene awataka wakenya kumshirikisha Ruto kwenye X Space

Wakenya wamealikwa kujiunga na mjadala wa X Space kuanzia saa nane mchana hadi saa kumi na moja jioni.

Muhtasari

•Charlene alitoa changamoto kwa vijana kukumbatia ishara ya Ruto ya kukutana nao katika harakati za kutatua tatizo zao.

•Rais William Ruto anatazamiwa  kuwa mwenyeji wa mazungumzo yake ya kwanza ya X-Space (zamani Twitter) na vijana wa Kenya mwendo wa saa nane mchana hadi saa kumi na moja jioni leo.

Charlene Ruto
Charlene Ruto
Image: Facebook

Binti wa kwanza Charlene Ruto amewataka vijana kujiunga na mkutano wa mtandao wa X Space na Rais William Ruto ili kueleza wasiwasi wao kufuatia maandamano ya hivi majuzi yaliyokumba maeneo kadhaa nchini.

Katika taarifa yake kupitia mtandao wa X , Charlene alitoa changamoto kwa vijana kukumbatia ishara ya Ruto ya kukutana nao katika harakati za kutatua changamoto za maandamano.

"Vijana, nafasi ya maisha inawangojea. Ninawahimiza kuitumia kwa busara na kushiriki kwa njia yenye kujenga kwa sababu nyinyi ndio mtakaoamua mwendelezo wa viwango hivyo vya mijadala kwa mafanikio yenu,” Charlene alisema.

Rais William Ruto anatazamiwa  kuwa mwenyeji wa mazungumzo yake ya kwanza ya X-Space (zamani Twitter) na vijana wa Kenya mwendo wa saa nane mchana hadi saa kumi na moja jioni leo.

Kulingana na Ikulu, baraza la mawaziri limepangwa kujiunga na majadiliano ya mtandaoni ya saa tatu. 'X Spaces', ni kipengele kinachokuruhusu kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja ya sauti kwenye jukwaa la mitandao ya kijamii.

Tangazo hilo lilitolewa katika vyombo vya habari baada ya kikao cha baraza la mawaziri kilichoongozwa na rais kwenye  Ikulu ,Alhamisi Julai 5 ,2024.

Wakenya wamealikwa kujiunga na mjadala wa X Space kuanzia saa nane mchana hadi saa kumi na moja jioni.

"Wakenya wote wanakaribishwa kuchangia mazungumzo haya kama sehemu ya juhudi zetu za pamoja za kukuza upya wa kitaifa na kuunda Kenya bora kwa wote," 

Maendeleo hayo yanakuja kufuatia maandamano ya Gen Zs kushinikiza mageuzi ya utawala. Maandamano ya awali ya kitaifa dhidi ya mswada wa fedha wa 2024 ambao umetupiliwa mbali, yalishuhudia maelfu ya vijana wa Kenya wakiingia mitaani kwa wiki mbili.

Katika mahojiano ya pamoja ya wanahabari kwenye televisheni hapo awali, mkuu wa nchi alisema yuko tayari kuwashirikisha vijana kwenye jukwaa analopenda.