Kiongozi wa Azimio Raila Odinga ameomba radhi kwa wanahabari baada ya wanahabari kukasirishwa na wahuni katika hafla yake iliyofanyika katika afisi za Jaramogi Oginga Odinga Foundation (JOOF).
Wakati wa tukio hilo viongozi kutoka vyama vingine vinavyounda Azimio pia walikasirishwa na vijana hao wenye ghasia.
Raila katika taarifa yake Alhamisi asubuhi aliwahakikishia wanahabari na viongozi waliokuwepo wakati wa kisa hicho cha kusikitisha kwamba chama chake kitawachukulia hatua wahusika.
“Mheshimiwa Raila Odinga anajutia matukio ya jana (Jumatano) na anachukua fursa hii mapema kuwaomba radhi wanahabari na viongozi wenzake walionaswa na tukio hilo la kusikitisha."
“Mhe.Odinga anawahakikishia wanahabari na viongozi wenzake kwamba umoja huo utafanya uchunguzi wa matukio na kuziba mianya iliyosababisha uvunjifu wa usalama kwa nia ya kuhakikisha wanahabari na viongozi wanakuwa salama na huru katika shughuli zote za Azimio, zikiwemo zile za mkutano wa hadhara," msemaji wake Dennis Onyango alisema.
Vijana waliojaa hamaki walivuruga mkutano uliokuwa ufanyike baina ya viongozi wa Azimio na wanahabari Jumatano,Julai 17,2024.
Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alikuwa akihutubia wanahabari wakati vijana, zaidi ya 50 walipovamia hema wakidai hawataruhusu kiongozi yeyote kumvunjia heshima Raila.
"Hakuna anayemdharau Raila tukiwa hai, hakuna mkutano na wanahabari hapa," vijana hao walifoka huku wakigeuza viti juu chini.