Gavana wa Elgeyo Marakwet amsihi rais Ruto kumrudisha Murkomen katika baraza la mawaziri

Katika baraza lake jipya, rais Ruto aliwarudisha mawaziri wa zamani 4 kazini, wengine katika wizara walizokuwa wakishikilia na wengine katika wizara tofauti.

Muhtasari

• Aidha, katika kundi hilo la kwanza kwenye baraza jipya la watu 11, mawaziri wateule 5 walikuwa ni majina mapya.

• Rais Ruto anatarajiwa kuteua mawaziri zaidi kwenye wizara mbalimbali kama vile michezo, kawi na wizara zingine wiki kesho.

Siku moja baada ya rais William Ruto kutangaza kundi la kwanza la baraza jipya la mawaziri, gavana wa kaunti ya Elgeyo Marakwet, Wisley Rotich amemuomba mkuu wa nchi pia asimsahau aliyekuwa waziri wa barabara na uchukuzi, Kipchumba Murkomen.

Rotich kupitia ukurasa wake wa Facebook, aliwapongeza wote walioteuliwa kisha akamsihi rais Ruto kumfikiria upya pia waziri huyo wa zamani, akisema kwamba ana uwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu ya kiserikali.

“Tunawapongeza wote walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali za CS na kuwatakia heri. Kwa unyenyekevu wa hali ya juu bado tunaamini kuwa MHE Rais atamzingatia Mwana wetu wa EMC Onesimus Kipchumba Murkomen kwenye baraza la mawaziri kulingana na umahiri wake, bidii na uwezo wake wa kutumikia Kenya. Kwa Mungu tunamtumaini,” Rotich alisema.

Rais Ruto alitangaza kulivunja baraza lake la mawaziri mnamo Julai 11 na kuwatuma mawaziri wote nyumbani.

Katika baraza lake jipya, rais Ruto aliwarudisha mawaziri wa zamani 4 kazini, wengine katika wizara walizokuwa wakishikilia na wengine katika wizara tofauti.

Baadhi ya waliorudishwa katika nyadhifa zao za awali ni pamoja na Kithire Kindiki wa usalama wa ndani, Aden Duale wa ulinzi, Soipan Tuya wa mazingira na Alice Wahome wa ardhi.

Wenzao Davis Chirchir aliyekuwa katika wizara ya kawi aliteuliwa katika wizara ya barabara na uchukuzi huku Rebecca Miano aliyekuwa katika wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda akiteuliwa kama mwanasheria mku wa serikali.

Aidha, katika kundi hilo la kwanza kwenye baraza jipya la watu 11, mawaziri wateule 5 walikuwa ni majina mapya.

Rais Ruto anatarajiwa kuteua mawaziri zaidi kwenye wizara mbalimbali kama vile michezo, kawi na wizara zingine wiki kesho.