Gavana Nassir amsihi Ruto kuondoa kesi dhidi ya waandamanaji

Mkuu huyo wa kaunti alimtaka Rais kuondoa kesi za wote waliokamatwa wakati wa maandamano hayo.

Muhtasari
  • Nassir alimweleza Ruto kuwa wale waliojeruhiwa na kuuawa wakati wa maandamano hayo pia lazima walipwe fidia.
Image: PCS

Gavana wa Mombasa Abdullswamad Sheriff Nassir amemtaka Rais William Ruto kutimiza ahadi yake kwa wananchi kwa kuhakikisha kesi zote zinazowasilishwa dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali zinatupiliwa mbali.

Akizungumza wakati wa utoaji wa ruzuku kwa makundi mbalimbali ya wavuvi kutoka Mombasa na viunga vyake, Nassir alimweleza Ruto kuwa wale waliojeruhiwa na kuuawa wakati wa maandamano hayo pia lazima walipwe fidia.

"Mheshimiwa nimekusikia na pia nimesikia maneno ya kiongozi wa chama changu Raila Amollo Odinga, waliojeruhiwa na kuuawa wakati wa maandamano lazima walipwe. Hatua pia zichukuliwe dhidi ya wale maafisa wa polisi waliotumia nguvu kupita kiasi," alisema.

Mkuu huyo wa kaunti alimtaka Rais kuondoa kesi za wote waliokamatwa wakati wa maandamano hayo.

"Kuwa mwaminifu kwa neno lako na ninajua kuwa utafanya hivyo. Ondoa kesi dhidi ya waliokamatwa," Nassir aliongeza.

Mnamo Jumatano, Ruto alikubali matakwa ya Upinzani kuwataka wote waliokamatwa wakati wa maandamano ya hivi majuzi waachiliwe.

Ruto aliagiza vyombo vya usalama kutii agizo hilo.

Mkuu wa Nchi wakati huo huo aliamuru mashtaka yote yaliyoshinikizwa dhidi yao yatupwe.

“Ninaviomba Vyombo vya Haki za Jinai kuchukua hatua madhubuti na kuhakikisha watu ambao wanaweza kuwa wamekamatwa bila hatia katika upande mbaya waachiliwe na kufunguliwa mashtaka,” alisema.

Ruto yuko eneo la pwani kwa ziara ya kimaendeleo katika kaunti za Mombasa na Kilifi.

Ameandamana na Magavana Abdullswamad Nassir (Mombasa), Fatuma Achani (Kwale), Waziri wa zamani Aisha Jumwa, Issa Timamy (Lamu), Godhana Dhadho (Tana River), wabunge na MCAs.