Sakaja alazimika kutoroshwa kutoka soko la Toi huko Kibra

"Hitilafu ya umeme katika moja ya nyumba za mbao imesababisha moto huo mapema leo asubuhi," mmoja wa wafanyabiashara alisema.

Muhtasari

• "Hitilafu ya umeme katika moja ya nyumba za mbao imesababisha moto huo mapema leo asubuhi," mmoja wa wafanyabiashara alisema.

• Watu wanne waliripotiwa kuteketea kiasi cha kutotambulika kufuatia moto ulioteketeza soko la Toi.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alilazimika kutoroshwa kutoka soko la Toi huko Kibra huku wakazi wakionekana wakirusha mawe.

Katika video iliyoonekana na gazeti la Star Jumamosi, watu walisikika wakimzomea huku mawe yakirushwa kuelekea kwake.

Usalama wake ulilazimika kumkinga gavana alipokuwa akiondoka sokoni. Sakaja alikuwa ametembelea soko kufuatia moto huo asubuhi ya leo.

Moto huo unaoaminika kuanza mwendo wa saa nne asubuhi Jumamosi, unashukiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme.

"Hitilafu ya umeme katika moja ya nyumba za mbao imesababisha moto huo mapema leo asubuhi," mmoja wa wafanyabiashara alisema.

Watu wanne waliripotiwa kuteketea kiasi cha kutotambulika kufuatia moto ulioteketeza soko la Toi.

Mtoto alikuwa miongoni mwa wale wanne. Waathiriwa walikuwa wakijaribu kuokoa mali zao walipozidiwa nguvu na moto huo.

Moto huo uliathiri wafanyabiashara wasiopungua 2,000, na kuwaacha wengi wakihesabu hasara zao. Mwenyekiti wa Soko la Toi Kenneth Jumba alisema anashuku moto huo uliwashwa kimakusudi.

"Hatujawahi kupokea ripoti kuhusu kilichosababisha moto ambao tulikumbana nao mwaka jana. Tumewazoea," Kenneth alisema.

Wazima moto kutoka Serikali ya Kaunti ya Nairobi walifika saa chache baadaye moto huo ukisambaa kwa kasi.

Hii si mara ya kwanza kwa soko hilo kuteketea kwa moto. Soko limekuwa na mazoea ya kuwaka moto mara kwa mara.