Msemaji wa ikulu amtetea Ruto dhidi ya madai ya kuzindua upya miradi iliyozinduliwa na Uhuru

“Hivyo naam, katika ziara zake za maendeleo nchi nzima, Rais ataendelea kuzindua miradi mipya, kukagua inayoendelea, na pale inapobidi, kufufua na kukamilisha ile iliyokwama kabla ya kuchaguliwa kwake."

RAIS RUTO
RAIS RUTO
Image: FACEBOOK//WILLIAM RUTO

Msemaji wa ikulu ya Nairobi, Hussein Mohamed ametetea hatua ya rais William Ruto kuendeleza uzinduzi wa miradi ambayo baadhi ya Wakenya wameibua madai kwamba ni miradi iliyozinduliwa awali na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta.

Kupitia ukurasa wake wa X, Mohamed alionekana kulenga mkuki wake kwa gazeti la Standard ambalo taarifa yake kuu katika toleo ya Jumamosi 17, 2024 ilikuwa inazungumzia Ruto kuzindua miradi iliyozinduliwa awali.

Mohamed katika utetezi wake, akisema kwamba ni wajibu wa kiongozi wa taifa kuhakikisha miradi yote, iwe mipya au iwe ile iliyozinduliwa na kukwama inakamilika kwa faida ya wananchi wote.

“Ni alama ya wajibu kwa Rais kuhakikisha kwamba miradi yote inayowezekana, ikiwa ni pamoja na ile iliyokwama kabla ya kuchaguliwa kwake, inakamilika. Ahadi hii kwa hakika ni sehemu ya ahadi za Rais  @Williamsruto iliyotolewa katika manifesto ya Kenya Kwanza, hati yenyewe iliyomfanya achaguliwe,” Mohamed alisema.

Aliongeza kuwa hakuna hatia yoyote kwa rais kufuatilia miradi yote iliyogharimu pesa za mlipa ushuru na kuona imefikia wapi na kama ilikwama kuizindua upya ili kukamilika

“Hivyo naam, katika ziara zake za maendeleo nchi nzima, Rais ataendelea kutekeleza Ajenda ya Mabadiliko ya Uchumi ya Bottom-Up, ikiwa ni pamoja na kuzindua miradi mipya, kukagua inayoendelea, na pale inapobidi, kufufua na kukamilisha ile iliyokwama kabla ya kuchaguliwa kwake - YOTE. KWA FAIDA YA WANANCHI! Muwe na wikendi njema wadau,” aliongeza akiwataja Standard.

Katika ziara zake katika maeneo mbalimbali nchini zilizorejelewa baada ya miezi kama 2 ya maandamano ya Gen Z iliyomkwamisha Nairobi, Ruto ameonekana na kusikika akitoa ahadi chungu nzima, lakini pia akizindua miradi ya maendeleo mbalimbali.