logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Jinsi wafanyikazi wa Wells Fargo walitoroka na milioni 94 za supermarket maarufu -DCI

Maafisa wa usalama walipata lori tupu ambalo lilikuwa na pesa hizo likiwa limetelekezwa katika eneo la South C.

image
na Samuel Maina

Habari07 November 2023 - 07:05

Muhtasari


  • •DCI wameanzisha msako wa kuwasaka wafanyikazi wa Wells Fargo wanaodaiwa kutoroka na 94 milioni za duka kubwa maarufu.
  • •Maafisa wa usalama walipata lori tupu ambalo lilikuwa na pesa hizo likiwa limetelekezwa katika eneo la South C.

Makachero wa DCI wameanzisha msako mkubwa wa kuwasaka wafanyikazi wawili wa Wells Fargo wanaodaiwa kutoroka na Ksh 94 milioni za duka kubwa maarufu.

Daniel Mungai Mugetha ambaye ni kamanda wa kikosi na Anthony Nduiki Waigumu, dereva, wanaripotiwa kutoweka na kiasi hicho kikubwa cha pesa baada ya kuliacha gari la kampuni lililokuwa limebeba pesa hizo katika eneo la Dafarm eneo la South C, Nairobi.

Maafisa wa DCI wameripoti kuwa washukiwa waliendesha lori hilo kwa siri kutoka kwa afisi ya kampuni hiyo ya ulinzi jijini Nairobi muda mfupi baada ya pesa kupakiwa ndani. Inasemekana waliacha gari la polisi la kusindikiza lililokuwa likisubiri kuruhusiwa kuondoka.

“Bila kujua kwamba lori nambari. KBA 517T walilokuwa wasindikize lilikuwa limeondoka dakika za awali, timu ya wasindikizaji yenye silaha ilikwenda kuuliza kutoka kwa wasimamizi kwa nini upakiaji ulikuwa unachukua muda mrefu sana. Kufikia wakati huo, hakuna lori wala wafanyakazi walioweza kupatikana,” ilisoma ripoti ya DCI.

DCI waliongeza, “Ripoti ya Meneja wa Uchunguzi wa kampuni hiyo ilionyesha kuwa gari hilo aina ya Isuzu Canter lilikuwa likisafirisha pesa kwa benki moja iliyoko mtaa wa Kenyatta Avenue, Nairobi, na lilibeba Sh94 milioni za duka kubwa maarufu nchini.”

Maafisa wa polisi kutoka Lang’ata ambao walihamasishwa kuwatafuta washukiwa hao baadaye walipata lori tupu ambalo lilikuwa na pesa hizo likiwa limetelekezwa katika eneo la South C.

Maafisa wa upelelezi kutoka tawi maalum tangu wakati huo wameanzisha msako mkali wa kuwatafuta washukiwa na kurejesha pesa zilizoibwa.

DCI pia imetoa picha za washukiwa hao wawili na kuwataka umma kushiriki habari  muhimu zitakazosaidia kukamatwa kwao.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved