logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Seneta Cherargei asimulia kuibiwa akiwa kwenye 'jam' Nairobi

Nairobi sasa ni jiji la uhalifu na kimbilio la magenge - mwandani huyo wa Ruto alisema.

image
na Radio Jambo

Habari16 November 2022 - 08:38

Muhtasari


• Wiki mbili zilizopita nilipoteza kioo cha upande wa kushoto cha gari langu nikiwa nimekwama kwenye msongamano - Cherargei.

Seneta wa Nandi, Samson Cherargei

Huku wakaazi wa jiji kuu la Nairobi wakiendelea kulilia serikali kumaliza visa vya uhalifu na kuzima magenge ambayo yameibuka kuwashambulia watu, imebainika kuwa magenge hayo hayawasazi hata viongozi tajika katika serikali.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei kupitia ukurasa wake wa Twitter alielezea jinsi alivyofanyiwa madhira na jambazi mmoja katika barabara ya Valley viungani mwa jiji.

Cherargei alieleza kwamba alitazama bila msaada wowote jinsi mwizi huyo alikuwa anavunja kioo cha pembeni cha gari lake huku akiwa amekwama kwenye msongamano wa magari.

“Wiki mbili zilizopita nilipoteza kioo cha upande wa kushoto cha gari langu nikiwa nimekwama kwenye msongamano kwenye Barabara ya Valley kikiondolewa kwa nguvu na nduli. Nairobi sasa ni jiji la uhalifu na kimbilio la magenge. Kudorora kwa usalama kote nchini lazima kushughulikiwe mara moja na kupanga upya sekta ya usalama,” seneta Cherargei alieleza.

Suala la usalama jijini limekuwa likiwaogopesha wengi wa wakaazi haswa baada ya mikanda ya CCTV kusambazwa mitandaoni ikionesha jinsi magenge hayo yanawavamia wananchi wasio na uwezo wa kujilinda na kujitetea dhidi ya makali yao.

Ili kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa usalama katika mji mkuu, Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome mnamo Jumanne, Novemba 15, alimtaja Adamson Bungei kama kamanda wa polisi wa kaunti ya Nairobi.

Bungei, ambaye ni kamanda wa polisi wa kaunti ya Baringo, anachukua wadhifa huo kutoka kwa Manase Musyoka, ambaye alikuwa bado kushika wadhifa huo kufuatia mabadiliko yaliyofanywa hivi majuzi na aliyekuwa kaimu IG Nur Gabow katika wiki zilizopita.

Afisa huyo wa polisi wa Nairobi sasa ana jukumu la kukabiliana na ongezeko la uhalifu katika mji mkuu huo ambao ulisababisha malalamiko kutoka kwa umma.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved