"Wacheni upuzi!" Ruto awaambia MCAs wa Kericho baada ya kurushiana ngumi bungeni

MCAs hao walipigana wakati wa kikao cha kujadili bajeti ya ziada ambapo suala la vyeo katika bunge hilo liliibuka.

Muhtasari

Hiyo michezo ambayo mnaendelea sisi tunataka kila kiongozi ambaye amechaguliwa aanze kupanga mambo ya wananchi - Ruto.

Ruto awafokea MCAs wa Kericho
Ruto awafokea MCAs wa Kericho
Image: Facebook

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kaunti ya Kericho ilikuwa na kikao maalum kujadili bajeti ya ziada, kikao ambacho mwisho wa siku kiligeuka kuwa uwanja wa kupimana nguvu MCAs wakirushiana ngumi na mateke huku mashati yakichanika.

Kabla ya kikao hicho ambacho kilitarajiwa kuwa na majibizano makali, spika wa bunge la kaunti ya Kericho Dr Mutai Patrick aliwafurusha waandishi wa habari ambao hakutaka wahudhurie kikao hicho ili kunasa habari muhimu.

Baadae MCAs walikosa mwafaka na kupelekea kurishiana ngumi na kuchafuana vikali huku pande mbili hasimu zikigombeana nyadhifa za uongozi wa bunge hilo badala ya kujadili bajeti ya ziada kama ilivyokuwa dhamira ya kikao chenyewe.

Rais Ruto ambaye ni mkuu wa chama cha UDA ambacho wengi wa MCAs hao walichaguliwa nacho ameonesha kukasirika kwake na bunge a kaunti ya Kericho.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa ibada ya pamoja kutoka makanisa mbalimbali katika kaunti ya Bomet, rais Ruto aliwasuta MCAs hao huku akiwaambia kuwa ni wakati wanafaa kuweka tofauti zao pembeni na kuwafanyia wananchi kazi.

“Niliona pale Kericho bado wanang’ang’ana na mambo ya vyeo, huyu anatafuta hii, mwingine anataka ile. Mimi nataka niwaambie MCAs wa kaunti ya Kericho, wacheni upuzi. Hiyo michezo ambayo mnaendelea sisi tunataka kila kiongozi ambaye amechaguliwa aanze kupanga mambo ya wananchi, sio kupigania vyeo mpaka mnapoteza muda wa bunge mkipigana. Aibu kwenu!” Rais alifoka huku hasira zikiwa zimetanda panda la uso wake.

Taarifa za hivi punde zinahoji kuwa kamati ya adhabu ya chama cha UDA tayari imemtaka spika Mutai kujiwasilisha mbele yake ili kujibu mashtaka ya kushindwa kudhibiti bunge na kuruhusu madiwani kupigana.