Jalang'o avunja kimya baada ya kutimuliwa kutoka chama cha ODM

Jalang’o alijitia moyo kwa mstari wa Biblia ambao unazungumza kuhusu Mungu kuwasaidia watu wake kushinda majaribu.

Muhtasari

•Viongozi hao walitimuliwa kutoka ODM kwa madai ya utovu wa nidhamu na kukaidi msimamo wa chama.

•Kufuatia hatua hiyo, Jalang'o alizamia kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo alishiriki ujumbe wa kujitia moyo.

Image: INSTAGRAM// JALANG'O

Siku ya Jumatano, Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o na viongozi wengine wanne walifurushwa kutoka kwa chama cha ODM kufuatia mkutano wa cha wa NEC uliofanyika jijini Nairobi.

Jalang’o, Mbunge wa Gem Elisha Odhiambo, Mbunge wa Bondo Gideon Ochanda, Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi na seneta wa Kisumu Tom Ojienda wote walitimuliwa kutoka kwa chama hicho kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu, Raila Odinga kwa madai ya utovu wa nidhamu na kukaidi msimamo wa chama.

Kufuatia hatua hiyo, mtangazaji huyo wa zamani wa redio alizamia kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo alishiriki ujumbe wa kujitia moyo.

"Hakuna jaribio ambalo ni nzito sana kuinua!," Jalang'o aliandika.

Mbunge huyo wa muhula wa kwanza aliambatanisha taarifa yake na picha yake ya kumbukumbu ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana ambapo alionekana akiwa amebeba sanduku kubwa la ushahidi mahakamani wakati wa kesi ya Azimio la Umoja dhidi ya ushindi wa rais William Samoei Ruto.

Kuongeza kwenye kauli yake, Jalang’o pia alishiriki mstari wa Biblia kutoka kwa kitabu cha Wakorintho 10:3 ambao unazungumza kuhusu Mungu kuwasaidia watu Wake kushinda majaribu.

“Hakuna jarabio lililokupita ambalo si kawaida ya kwa wanadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hatawaacha mjaribiwe kupita mnavyoweza, bali pamoja na lile jaribio atatengeneza na mlango wa kutokea, ili mweze kulistahimili,” mstari huo wa Biblia unasema.

Katika taarifa yake, chama cha ODM kilisema kuwa waliwatimua viongozi hao watano kwani walipinga maazimio yaliyotolewa na chama.

“Wanachama hao wanakabiliwa na tuhuma za ukiukwaji wa Ibara ya 11 (1) (e) ya katiba ya chama na kifungu cha 14A cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2011 kwa kujihusisha na kuunga mkono shughuli za chama pinzani na kupinga maamuzi/maazimio halali yaliyotolewa na chama. vyombo vya chama, wachukuliwe kama wamejiuzulu kutoka chama,” ilisomeka taarifa hiyo.

"Chama kinaagizwa kuanza mchakato wa kuwaondoa kwenye daftari la chama."

Mkutano wa NEC ulioitishwa na Raila mwenyewe ilikuja takriban mwezi mmoja baada ya wanachama hao kufika mbele ya kamati inayoongozwa na Sihanya kujitetea kutokana na shutuma za utovu wa nidhamu