Baada ya kufurushwa ODM, Jalang'o akutana na Mama Ida, asisitiza bado yuko ODM

“Mama Ida ni kama dadangu, tunatoka katika sehemu moja na naweza kushiriki jukwaa moja na Mama Ida muda wowote kwa sababu ameniunga mkono mara nyingi sana." Jalang'o alisema.

Muhtasari

• Matatizo yake yalianza pale yeye na wenzake kutoka Nyanza walipoamua kukutana na Rais Ruto katika ikulu ya Nairobi.

• Hii ni licha ya chama hicho kusisitiza kutomtambua Ruto kama raia aliyechauliwa kwa njia halali.

Jalang'o
Jalang'o
Image: Facebook

Wiki moja baada ya kamati ya nidhamu ya chama cha ODM ikiongozwa na kinara wao Raila Odinga kuwafukuza chamani wabunge wanne – akiwemo Jalang’o - na seneta mmoja  kwa tuhuma za kukiuka kanuni za chama, mbunge huyo sasa amekutana na mkewe Odinga, Mama Ida.

Jalang’o ambaye ni mbunge wa Lang’ata alikutana na Mama Ida katika hafla ya kuzindua safari za ndege kutoka uwanja wa Wilson ulioko Lang’ata moja kwa moja kwenda Migori.

Katika video ambazo zimevujishwa mitandaoni, Jalang’o alionekana akisalimiana kwa furaha na Mama Ida, jambo ambalo lilizua mkanganyiko kwa baadhi ya wafuasi wa ODM waliotaka kubaini hali yake ya kisiasa haswa katika chama cha ODM.

“Mama Ida ni kama dadangu, tunatoka katika sehemu moja na pia hapa niko katika eneobunge langu. Naweza kuwa hapa muda wowote na naweza kushiriki jukwaa moja na Mama Ida muda wowote kwa sababu ameniunga mkono mara nyingi sana. Ifahamike kwamba mimi ni mwanachama wa ODM wa maisha na sioni nikitoka ODM muda wowote hivi karibuni,” Jalang’o alibainisha.

Mbunge huyo wa ODM amekuwa akiandamwa na matatizo kutoka kwa uongozi wa chama kilichompa tikiti ya ushindi kwenda bungeni katika uchaguzi wa mwaka jana Agosti.

Matatizo yake yalianza pale yeye na wenzake kutoka Nyanza walipoamua kukutana na Rais Ruto katika ikulu ya Nairobi licha ya chama hicho kusisitiza kutomtambua Ruto kama raia aliyechauliwa kwa njia halali.

Baadae kamati ya nidhamu ya chama hicho ilipoketi wiki jana iliafikiana kwa sauti moja kwamba watano hao walikwenda kinyume na kanuni za chama kwa kufanya ziara ikulu pasi na kufanya mashauriano na viongozi wa chama hivyo kupendekeza kufurushwa kwao.

Hata hivyo, walielekea mahakamani na siku mbili zilizopita mahakama ya kusuluhisha mzozo wa uanachama ilisitisha agizo la kufurushwa kwao chamani ODM.

Odinga alikuwa ametaka kufurushwa kwao ili nyadhifa zao zitangazwe kuwa wazi na hivyo kutoa nafasi nyingine ya kuandaliwa kwa uchaguzi.