Familia ya mshukiwa wa mauaji ya Kware yazungumza,wafichua mambo kumhusu

Familia ya mshukiwa inasema kuwa hawajahi kumuona tangu mwaka wa 2022.

Muhtasari

•Mamake amefichua alimpeleka katika shule ya upili ya Uganda kwani hakuweza kupata pesa za kumpeleka shule aliyokuwa ameitwa Kenya.

•Ndugu za mtuhumiwa wanasema wanashangazwa sana na vitendo ambavyo kaka yao anatuhumiwa kutekeleza.

ambaye anashukiwa kuua wanawake kadhaa na kutupa miili yao katika eneo la kutupa taka la Kware, Mukuru kwa Njenga.
Collins Jumaisi ambaye anashukiwa kuua wanawake kadhaa na kutupa miili yao katika eneo la kutupa taka la Kware, Mukuru kwa Njenga.
Image: HISANI

Familia ya mshukiwa mkuu wa mauaji ya Kware, Collins Jumaisi,  imevunja ukimya na kufichua maelezo yasiyojulikana sana kuhusu maisha yake.

Mshukiwa huyo ambaye kwa sasa anazuiliwa kwa siku 30 huku uchunguzi ukiendelea alizaliwa Februari 1991 katika eneo la Hamisi, Kaunti ya Vihiga.

Baadaye alihamia kaunti ya Migori pamoja na mama yake na ndugu zake watatu baada ya baba yao kufariki mwaka wa 1995.

“Babake alikuwa anaitwa Elijah Jumaisi. Alinioa mwaka wa 79 akafa mwaka wa 85,” Bi Magret Rose Jumaisi, mamake mshukiwa, aliambia Citizen TV kwenye mahojiano.

Bi Margret alifichua maelezo kuhusu elimu ya Jumaisi akifichua kwamba alimpeleka katika shule ya upili ya Uganda kwa vile hakuweza kukusanya pesa za kutosha kumpeleka katika shule aliyokuwa ameitwa nchini Kenya baada ya kupita mtihani wa darasa la nane.

“Alisoma huko (Uganda) miaka tatu. Miaka mitatu hiyo, mimi nikaacha huko nikarudi Busia penye nilikuwa naishi. Vile nilienda Uganda sikumpata, nilipata ametoroka na mwenzake wamekuja Nairobi,” alisema.

Dada na kaka wa mtuhumiwa huyo wanasema wanashangazwa sana na mambo ambayo wanasikia kaka yao akituhumiwa kuyafanya.

Bw Ruebena Elijah Muhanji, ambaye ni kaka ya mshukiwa ametaka uchunguzi wa kina ufanywe ili kubaini kama kweli ndugu yao ndiye aliyehusika na mauaji ya wanawake ambao miili yao ilipatikana imetupwa katika eneo la Kware, mtaa wa Mukuru kwa Njenga.

“Kitendo ambacho ametenda ni kibaya mno, kibaya ambacho mimi siwezi sema afanywe hivi ama vile. Ila naomba serikali ifanye uchunguzi ijulikane kwamba ni ukweli ama si ukweli,” Elijah alisema.

Familia ya mshukiwa inasema kuwa ametoweka tangu mwaka wa 2022, huku mamake akidai kuwa wakati fulani alifikiri mwanawe alifariki.