Wapiga mbizi katika Bahari ya Baltic wamegundua meli ya mizigo ya karne ya 19, "iliyosheheni" shampeni, mvinyo, maji ya chupa na vyombo vya kauri.
Wanasema kuwa waliona kwa mara ya kwanza meli hiyo iliyozama kupitia kifaa cha kuchora ramani na kuchunguza bahari (Sonar) na walidhani ilikuwa mashua ya uvuvi.
Wanasema walipofika walihesabu zaidi ya chupa 100 za shampeni katika meli hiyo iliyozama pwani ya Sweden.
Na sasa Tomasz Stachura wa kikundi cha wapiga mbizi cha Baltitech, anaamini shehena hiyo inaweza kuwa ilikuwa inaelekea kwa mtawala mkuu wa Urusi.
Baltitech, ambayo inajihusisha na utafiti wa meli zilizozama katika Bahari ya Baltic inasema hiyo ni kama "hazina".
Bwana Stachura alisema "Nimekuwa mpiga mbizi kwa miaka 40. Mara nyingi unaweza kuona chupa moja au mbili. Lakini sijawahi kuona masanduku na chupa za pombe na chupa zenye maji, kama hivi."
Chupa za maji za udongo, zenye jina la kampuni ya Kijerumani Selters, ziliwasaidia kutambua mwaka wa meli hiyo kuwa ni kati ya 1850 na 1867.
Kulingana na hali ya vifuniko, shampeni hiyo inaweza kuwa bado "ina ladha nzuri" ingawa inaweza kuwa imeshapoteza kabisa gesi yake hadi sasa.