logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ulanguzi wa watoto; Naibu mkurugenzi wa matibabu wa NMS aachiliwa kwa dhamana

Naibu mkurugenzi wa matibabu wa NMS wachiliwa dhamana

image
na Radio Jambo

Yanayojiri25 November 2020 - 08:45

Muhtasari


• Mohammed  alishtakiwa kwa makosa mawili ya ulanguzi wa watoto.

• Mohammed anashtumiwa kwa kushirikiana na wengine kulangua watoto katika ya Mama Lucy.

• Kesi yao itatajwa Disemba 9

Mahakama

Naibu mkurugenzi wa  huduma za matibabu katika shirika linalosimamia kaunti ya Nairobi (NMS), Musa Mohammed ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki mbili pesa taslimu au dhamana ya shilingi laki tano na hakikisho katika kesi ya ulanguzi wa watoto.

Mohammed siku ya Jumatano alishtakiwa kwa makosa mawili ya ulanguzi wa watoto.

Mohammed ambaye alifika mahakamani akiwa kwenye kiti cha magurudumu anashtumiwa kwa kushirikiana na Fred Makallah na Sellina Awuor na idara ya wafanyikazi wa kijamii katika hospitali ya mama Lucy kulangua watoto katika hospitali hiyo kati ya  Machi Mosi na Novemba 16, 2020 katika hospitali ya Mama Lucy.

Makallah anakabiliwa na jumla ya mashtaka matano na aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja pesa taslimu au dhamana ya shilingi milioni mbili na hakikisho.

Mshtakiwa mwingine Selina Awuor aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki mbili pesa taslimu au dhamana ya shilingi laki tano na hakikisho.

Mohamed alishtakiwa kwa shtaka la pili la kushirikiana na Awuor akifahami fika kwamba Makallah alikuwa na jukumu maalum la kulangua watoto kutoka hospitalini na kukosa kutumia mamlaka yake kuzuia ulanguzi huo.

Alikuwa ajibu mashtaka dhidi yake siku ya Jumatatu lakini wakili wake aliambia mahakama kwamba alikuwa amelazwa katika hospitali kuu ya Kenyatta. Mohammed alikanusha  mshtaka dhidi yake mbele ya hakimu mkuu Martha Matuku.

Makallah na Awuor walishtakiwa siku ya Jumatatu.

Kesi yao itatajwa Disemba 9.

Siku ya Jumatatu afisa mkuu mtendaji wa hospitali hiyo Emma Mutiso aliachiliwa huru pamoja na maafisa wengine wa hospitali hiyo Juliana Mbete msimamizi wa hospitali, Beatrice Njambi mkuu wa kitengo cha watoto wachanga na afisa wa utawala Regina Musembi.

Makallah anadaiwa kufichuliwa na shirika la habari la BBC akipiga bei na mwanahabari mpekuzi katika sakata ya uuzaji wa watoto wanaochwa au kutelekezwa katika hospitali ya Mama Lucy.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved