Washirika wa naibu wa rais William Ruto kutoka Rift Valley wamemkosoa vikali rais Uhuru Kenyatta kwa kumshambulia Ruto hadharani baada ya Kenyatta kumtaka Ruto ajiuzulu kutoka serikalini badala ya kuihujumu akiwa ndani .
Wabunge Caleb Kostany na Oscar Sudi s wamesema rais hana mamlaka ya kumfuta kazi naibu wake na mashambulizi hayo dhidi ya Ruto hayafai kwani naibu wake hajamkosea heshima .
Sudi amesema wawili hao watasalia serikalini licha ya kuwepo tofauti kati yao hadi wakenya wapige kura kuamua atakayechukua usikani wa nchi mwaka ujao .
Ijumaa iliyopita rais Uhuru Kenyatta alionekana kumshambulia naibu wake kwa kumtaka ajizulu kutoka serikali badala ya kuikosoa na wakati mwingine kujisifia baadhi ya mafanikio ya serikali ambayo bado anaikosoa . Ruto kwa upande wake alisema hajamkosea heshima rais na ataendelea kuhudumu katika wadhifa wake kwani nafasi yake imelindwa na katiba licha ya kuwa majukumu yake yamekabidhiwa watu wengine . Ruto ameendelea na kampeini za kujipigia debe ili kumrithi rais Uhuru ambaye ameonekana kubadilisha msimamo wake kuhusu kumuunga mkono katika uchaguzi wa 2022 ili achukue usukani wakati muhula wake wa pili utakapotamatika .
Tofauti kati ya viongozi hao wawili wa Jubilee imezidishwa na misimamo yao tofauti kuhusu Ripoti ya BBI ambayo ais anaiunga mkono akiwa na mshirika wake mpya wa kisiasa Raila Odinga lakini inapingwa vikali na Ruto anayeshikilia kwamba katiba ya mwaka wa 2010 haifai kurekebishwa . Ruto na washirika wake wanahisi kwamba marekebisho hayo ya katiba yanalenga kumzuia kuchukua hatamu za uongozi kutoka kwa Uhuru ambaye alikuwa ameahidi kumpiga jeki Ruto ahudumu kipindi cha miaka 10 kama rais .