Wabunge Gladys Wanga na Lilian Gogo nusra wazabane makonde

Muhtasari

• Gogo alidai kuwa Wanga ana mazoea ya kuzuru eneo bunge lake na kuzindua miradi ya maendeleo bila yeye kujua.

• Gogo alisema huu ulikuwa mpango wa kisiasa uliopangwa na Wanga kudhoofisha rekodi yake ya maendeleo.

Mbunge wa Rongo Lillian Gogo
Mbunge wa Rongo Lillian Gogo
Image: Manuel Odeny

Mwakilishi wa kike wa Homa Bay Gladys Wanga nusra azabane makonde na mbunge wa Rangwe Lilian Gogo huku ubabe wa udhibiti wa kaunti ukijipenyeza hadi Bungeni.

Wabunge hao wawili ambao wamekuwa na tofauti za muda mrefu, walirushiana cheche za maneno kwenye sakafu ya Bunge na nusra wanyanyuane mbele ya spika wa bunge.

Gogo alidai kuwa Wanga ana mazoea ya kuzuru eneo bunge lake na kuzindua miradi ya maendeleo bila yeye kujua.

Kiini cha mzozo ni kwamba wakati wa kuzindua miradi, Wanga amekuwa akichukua sifa, akiwaambia wapiga kura wa Gogo kwamba ni yeye amezileta kutoka kwa serikali ya kitaifa.

Hatua hii haijamfurahisha Gogo, ambaye amedai kuwa hatua ya Wanga inakusudiwa kumwonesha kama mtu asiyekuwa na uwezo wa kushawishi serikali ili miradi ya maendeleo kutoka Nairobi.

 Gogo alisema huu ulikuwa mpango wa kisiasa uliopangwa na Wanga kudhoofisha rekodi yake ya maendeleo na kuchochea wapiga kura dhidi ya azma yake  ya kuchaguliwa tena mnamo 2022.

Jana, Gogo, alimtaka Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amzuie Wanga kudhoofisha katika eneo bunge.

"Ninasema kwamba ikiwa [Muturi] hautashughulikia suala la Gladys Wanga kunitusi katika eneo bunge langu, basi mambo hayatakuwa mazuri kwa bunge hili, "Gogo alifoka.

Gogo, alimlalamikia Spika kwamba mienendo ya Wanga ilikuwa potovu na haikwa hulka nzuri kwa bunge.

Mapema Gogo na Wanga walikuwa wamewasilisha malalamiko tofauti rasmi katika ofisi ya Spika wakituhumiana kwa kudhoofisha kazi ya kila mmoja.

Wanga kwa hamaki aliinuka na kusisitiza kwamba Spika ampe nafasi ya kujibu Gogo kuhusu madai yake.

Hata hivyo, Muturi alisema suala hilo sasa litachukuliwa na kamati ya maslahi ya Bunge ambapo watahitajika kujitetea.