Mwalimu mkuu aliyekamatwa kwa madai ya wizi mtihani aachiliwa kwa dhamana

Muhtasari

• Betta Mutuku ameachiliwa kwa dhamana ya polisi wakisubiri ripoti kutoka kwa wataalam wa uhalifu wa mtandao.

• Mutuku ambaye ni mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari ya ABC Kiseveni iliyoko kaunti ya Machakos alikamatwa na maafisa wa DCI Jumanne asubuhi.

Afisa mkuu wa DCI Machakos Rhoda Kanyi (kushoto) akiandamana na mwalimu mkuu wa shule ya ABC Kiseveni Betta Mutuku Aprili 6, 2021.
Afisa mkuu wa DCI Machakos Rhoda Kanyi (kushoto) akiandamana na mwalimu mkuu wa shule ya ABC Kiseveni Betta Mutuku Aprili 6, 2021.
Image: GEORGE OWITI

Mwalimu mkuu ambaye alikamatwa kwa madai ya wizi wa mtihani ya KCSE katika Kaunti ya Machakos ameachiliwa kwa dhamana ya polisi.

Afisa wa upelelezi wa jinai wa Machakos Rhoda Kanyi alisema mshukiwa aliachiliwa kwa dhamana huku wakisubiri wapelelezi wa uhalifu wa mitandao kumaliza uchunguzi kwenye simu yake iliyokamatwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

"Mwalimu mkuu ameachiliwa leo kwa dhamana ya polisi wakati tunasubiri ripoti kutoka kwa wataalam wa uhalifu wa mtandao," Kanyi aliwaambia waandishi wa habari Jumatano.

Betta Mutuku ambaye ni mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari ya ABC Kiseveni iliyoko kaunti ya Machakos alikamatwa na maafisa wa DCI Jumanne asubuhi.

Wapelelezi waliongozwa na Afisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Machakos Rhoda Kanyi ambaye alisema walimkamata baada ya kufuatilia habari za ujasusi.

Kanyi alisema mkuu huyo anashukiwa kuchukua picha ya karatasi ya mtihani ya KCSE na kuipakia kwenye ukurasa wake wa WhatsApp kwa watahiniwa kusoma.

Mshukiwa huyo alipelekwa kwenye kituo cha polisi cha Machakos ambapo alihojiwa na maafisa wa CID.

"Alikuwa ameweka mtihani kwa ukurasa wake kwa watahiniwa kusoma usiku," Kanyi aliwaambia waandishi wa habari wakati wa kukamatwa kwa mwalimu huyo.

Simu ya mkuu wa shule ilichukuliwa na maafisa wa polisi kusaidia katika uchunguzi.