Kenya yaunda jopo kushughulikia uhaba wa oksijeni

Muhtasari

• Kikosi kazi kinajukumu la kuweka mikakati ya muda mrefu pamoja na kutathmini miundombinu na uwezo wa kila hospitali kushughulikia hali hii.

• Kutokana na kuongezeka kwa wanaohitaji oksijeni nchini, mahitaji ya bidhaa hiyo yalipanda hadi tani 560 mwezi Januari na kwa sasa  mahitaji yanaelekea mara mbili ya mwaka jana kwa tani 880.

Mhasiriwa wa Covid-19 akiwa kwenye oksijeni
Mhasiriwa wa Covid-19 akiwa kwenye oksijeni
Image: HISANI

Wizara ya Afya imeunda 'Kikosi Kazi cha Oksijeni' ili kukabiliana na uhaba wa mitungi ya gesi hiyo nchini wakati wa janga la Covid-19.

Kikosi kazi kinajukumu la kuweka mikakati ya muda mrefu pamoja na kutathmini miundombinu na uwezo wa kila hospitali kushughulikia hali hii.

Waliratibu maswala ya huduma, ukarabati na kuweka mabomba ya ya gesi kama vigezo vikuu vya kukidhi mahitaji.

"Wahudumu wote katika sekta hii wanafanya bidii kushughulikia uhaba huo na kuhakikisha kuwa oksijeni inapatikana," Wizara ilisema.

Serikali imelazimika kuchukuwa hatua za haraka kuimarisha usambazaji wa oksijeni katika hospitali kutokana na hofu ya uhaba wa hewa hiyo muhimu katika mahospitali.

Kulingana na Wizara ya Afya, uzalishaji na mahitaji ya oksijeni ulikuwa takriban tani 410 kulingana na mahitaji ya mwaka jana.

Lakini kutokana na kuongezeka kwa visa vya wagonjwa mahututi wanaohitaji oksijeni nchini, mahitaji ya bidhaa hiyo yalipanda hadi tani 560 mwezi Januari na kwa sasa mahitaji yanaelekea mara mbili ya mwaka jana kwa tani 880.

"Mahitaji ya oksijeni ni ya juu kwa sababu ya Covid-19. Lakini tunashirikiana na washirika na wauzaji kushughulikia hali hiyo," wizara ilisema.

Serikali imewataka watu wanaoshikilia mitungi ya oksijeni nyumbani, ile ambayo haitumiki katika vituo vya afya na taasisi zingine kuitoa kuruhusu kujazwa tena ili itumike na wanaohitaji.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya mitungi elfu ishirini imeshikiliwa katika maeneo mbali mbali nchini.

 

Kila mtungi unagharimu takriban Shilingi 40,000.