Rais Samia Suluhu kufanya ziara ya kikazi nchini Kenya

Muhtasari

Akiwa nchini Kenya  atafanya mazungumzo na  Rais Uhuru Kenyatta kisha atalihutubia Bunge la Kenya litakalojumuisha Wabunge wa Mabunge yote mawili ya nchi hiyo. 

Image: IKULU TANZANIA

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, atafanya ziara ya kikazi nchini Kenya siku ya Jumanne.

Rais Samia atakuwa katika ziara nchini humo kwa siku mbili ambapo atapokelewa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Akiwa nchini humo atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Kenyatta kisha atalihutubia Bunge la Kenya litakalojumuisha Wabunge wa Mabunge yote mawili ya nchi hiyo. Taarifa ya Ikulu nchini Tanzania imeeleza.

Aidha, Rais Samia atahudhuria na kuhutubia mkutano wa jukwaa la wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania utakaofanyika jijini Nairobi kwa lengo la kujadiliana masuala yahusuyo fursa za kibiashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania na Kenya.

Hii ni safari ya pili kwa rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania tangu kuchukua madaraka baada ya kifo cha Hayati Dkt John Pombe Magufuli.

Alifanya safari yake ya kwanza kama Rais nchini Uganda mnamo Aprili 11 na Rais Yoweri Museveni akielezea kuwa lengo la ziara yake ni kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na kumaliza makubaliano ya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka nchini Uganda.

Uganda na Tanzania zilisaini mikataba mitatu yenye nia ya kuendeleza sekta ya mafuta na gesi ya Uganda, wakati wa ziara ya hiyo.

Image: MUSEVENI-TWITTER

Serikali hizo zilikubaliana katika masuala ya hisa, usafirishaji na ushuru katika hatua za awali za mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki.

Ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi una jumla ya Kilometa 1,443 kutoka Magharibi mwa Uganda mpaka kwenye bandari ya bahari ya Hindi, Tanga.

Kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia

Rais Samia Suluhu aliahidi kuwa serikali yake itasimamia kwa umakini suala la uhusiano baina ya Tanzania na nchi jirani na kuwa chachu ya kujenga jamii bora baina ya mataifa hayo.

"Kwa jirani zetu na marafiki zetu niwahakikishie tutaulipa wema mliotuonesha kwa kuimarisha na kushamirisha uhusiano wetu nanyi," alisema Rais Suluhu katika hotuba yake ya kumuaga Hayati Magufuli mkoani Dodoma.

Pia ujumbe huo unaleta majibu ya swali la mustakabali wa Kidiplomasia wa Tanzania na Jumuiya ya kimataifa.

Kwamba Rais amethibitisha kuwa yupo tayari kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwaita "Marafiki zetu" ikiwa na maana ya kuwakaribisha katika mashauriano ya Kidiplomasia na kuwahakikishia ushirikiano madhubuti.