FRANCIS ATWOLI ROAD!

Matendo ya Mungu ni Makuu! Atwoli ajibu wanaomuonea wivu

Atwoli amekanusha madai kuwa bango la 'Francis Atwoli Road' limeng'olewa huku akiagiza wanaoeneza uvumi huo kuacha kupoteza wakati wao.

Muhtasari

•Atwoli amekanusha madai kuwa bango hilo limeng'olewa huku akiagiza wanaoeneza uvumi huo kuacha kupoteza wakati wao.

•Atwoli pia alimkashifu vikali wakili tajika Ahmednasir Abdullahi almaarufu kama Grand Mulla kwa kusema kuwa kupatia barabara jina la Atwoli ni aibu kubwa.

Francis Atwoli akizungumza kwenye hafla ya kuzindua barabara ya Francis Atwoli Road
Francis Atwoli akizungumza kwenye hafla ya kuzindua barabara ya Francis Atwoli Road
Image: Hisani

Serikali ya kaunti ya Naorobi ilibadilisha jina la barabara ya Dik Dik iliyo eneo la Kileleshwa na kuipa jina mpya 'Francis Atwoli Road' siku ya Alhamisi.

Katibu mkuu wa COTU alipongeza serikali hiyo kwa kile alichoita kuheshimu wafanyikazi wote na viongozi wa miungano ya wafanyikazi walioaga. Hata hivyo, uzinduzi wa barabara hiyo haukupokelewa kwa furaha na maelfu ya Wakenya mitandaoni huku wakikashifu na kukejeli hatua hiyo.

Baadhi ya wanamitandao walikuwa wametishia kung'oa bango lililoonyesha jina mpya ya barabara hiyo huku picha ya bango lile likiwa imebebwa na lori ikisambazwa mitandaoni ikisemekana kuwa lilikuwa limengolewa na wananchi wenye ghadhabu punde baada ya kuwekwa.

Atwoli amekanusha madai kuwa bango hilo limeng'olewa huku akiagiza wanaoeneza uvumi huo kuacha kupoteza wakati wao. Radio Jambo pia imethibitisha kuwa bango hilo bado limo. Picha inayozunguka mitandaoni ikionyesha bango hilo likiwa kwa lori imeripotiwa kupigwa wakati bango hilo lilikuwa linapelekwa kuwekwa pale.

"Hakuna kilichotolewa ili kuwafanya mfurahie, msipoteze muda mkisherehekea habari za uongo! Mapenzi ya Mungu ni makuu." Atwoli aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Kwa ujumbe mwingine kupitia akaunti ya COTU, muungano huo ulidai kuwa uvumi huo ulikuwa unaenezwa na mlengo wa kisiasa wa naibu rais almaarufu kama 'Hustler Nation'

"Wanachukia kazi kubwa na mafanikio ambayo ni ya kusifiwa . Katibu mkuu wa COTU amejitolea kuhudumia wafanyakazi wa Kenya, Afrika na dunia bila ubinafsi na jambo hilo limepokelewa na serikali ya Kaunti ya Nairobi." muungano  huo ulisema.

Atwoli pia alimkashifu vikali wakili tajika Ahmednasir Abdullahi almaarufu kama Grand Mulla kwa kusema kuwa kupatia barabara jina la Atwoli ni aibu kubwa. Grand Mulla alidai kuwa hatua hiyo ilikuwa ya kukejeli maskini kwani Atwoli hukula na kunywa na matajiri kuonyesha kiburi kwa maskini.

"Matendo yangu yanajiongelea . Tofauti na wewe, mimi ni mtu mwaminifu, natia bidii na sijihusishi na mipango ya ufisadi, naongea kilicho akilini mwangu na mimi sio bilionea kama wewe. Ushawishi wangu ni kutokana na kukuza muungano wa wafanyakazi nchini. Kazi za Wakenya zimelindwa" Atwoli alimjibu Nasir.