MAAFA KWALE

Kwale: Huzuni baada ya familia kupoteza mapacha baharini

Mili ya wawili hao ilipatikana mahala pamoja wakiwa wameshikana mikono

Muhtasari

•Kennedy Gichuri na Solomon Macharia walikuwa wameenda kuogelea na jamaa mmoja wakati maafa hayo yalitokea.

•Mapacha hao walikuwa wamemaliza masomo yao ya shule ya upili wakisubiria kujiunga na chuo kikuu. 

Diani Beach Kwale
Diani Beach Kwale
Image: SHABAN OMAR

Hali ya huzuni imetanda baina ya familia moja upande wa Kwale baada ya kupoteza mapacha wao waliozama majini walipokuwa wanaogelea kwenye ufuko wa Gazi ulio katika eneo bunge la Msambweni siku ya Jumapili.

Inadaiwa kuwa Kennedy Gichuri na Solomon Macharia walikuwa wameenda kuogelea na jamaa wakati maafa hayo yalitokea.

Wawili hao walikuwa na umri wa miaka 18 kila mmoja na jamaa aliyeokolewa ana umri wa miaka 14.

Tukio hilo lilitokea licha ya mikutano ya fuko za umma kupigwa marufuko kutokana na janga la Corona.

Samuel Gitundu Njuguna ambaye ni baba ya wawili hao alisema kuwa vijana hao waliwezwa na mikondo ya bahari walipokuwa wanajaribu kufika kwenye ufuo.

"Walikuwa wanaogelea mahala ambapo palikuwa juu kiasi ila walipojaribu kurudi wakajipata mahala penye kinana hawakuweza kutokea" Bw Gitundu alisema.

Imeripotiwa kuwa jamaa wa umri wa miaka 14 aliokolewa na mvuvi mmoja akiwa ameshikwa na mti. Hata hivyo, kwa wakati huo alikuwa amepoteza fahamu na hangeweza kupatiana ujumbe wowote kuhusiana na tukio hilo.

Mapacha hao walikuwa wamemaliza masomo yao ya shule ya upili wakisubiria kujiunga na chuo kikuu. Gichuri alikuwa amenyakua gredi C+ ilhali Macharia alikuwa amezoa gredi ya C kulingana na baba yao.

Mili ya wawili hao iliweza kupatikana asubuhi ya kuamkia Jumanne baada ya shughuli ya kutafuta ya masaa matatu iliyoanza saa kumi na moja asubuhi. Shughuli ya kutafuta miili ile ilifeli siku ya Jumatatu kutokana na giza na mawimbi makubwa.

Wawili hao walipatikana mahala pamoja wakiwa wameshikana mikono na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Kwale.

Familia imeanza kutayarisha mazishi ya mapacha hao.

Tafsiri imefanywa na Samuel Maina