Kijana mtunza nyumba aliyeteka nyara mjukuu wa mwajiri wake akamatwa

Katika juhudi zake za kuepuka kukamatwa, Kingori alikuwa ameenda kwa saluni na kusukwa nywele ili kuficha sura yake.

Muhtasari

•King'ori alikamatwa jioni ya Jumatatu alipokuwa anajaribu kutoroka kwa kutumia pikipiki masaa chache tu baada ya mtoto aliyedaiwa kuteka nyara kupatikana akiwa kwenye nyumba iliyotelekezwa mjini Naivasha.

Charles Kingori alias Delvin Maina baada ya kukamatwa mjini Naivasha, Jumatatu
Charles Kingori alias Delvin Maina baada ya kukamatwa mjini Naivasha, Jumatatu
Image: Hisani

Kijana mtunza nyumba aliyeshukiwa kuteka nyara mjukuu wa miaka 4 wa mwajiri wake anazuiliwa katika kituo cha polisi baada ya kukamatwa kwenye mitaa ya mji wa Naivasha.

Charles King'ori aliyejitambulisha kwa jina bandia kama Delvin Maina alikamatwa jioni ya Jumatatu alipokuwa anajaribu kutoroka kwa kutumia pikipiki masaa chache tu baada ya mtoto aliyekuwa ameteka nyara kupatikana ndani yanyumba iliyotelekezwa mjini Naivasha.

"Mshukiwa amekamatwa dakika chache tu zilizopita kufuatia uwindaji mkubwa ulioshuhudiwa na umma kwenye mitaa ya mji wa Naivasha. Kingori alikamatwa alipojaribu kuwakimbia maafisa waliokuwa wanamuwinda masaa chache tu baada ya mtoto aliyekuwa ameteka nyara kunusuriwa" Shirika la DCI lilitangaza siku ya Jumatatu.

Kingori anadaiwa kumteka nyara mtoto Liam Ngucwa Mwangi mwenye umri wa miaka nne siku ya Jumatano wiki iliyopita maeneo ya Murang'a. Familia ya Liam ilikuwa imefanya juhudi kubwa kumtafuta mtoto huyo huku tangazo za kuchapishwa zikisambazwa mitandaoni.

Liam alikuwa ameonekana kwa mara ya mwisho tarehe Juni 2 akiwa mikononi mwa Kingori maeneo ya Gatunyu, Thika.

Katika juhudi zake kuzuia kukamatwa, Kingori alikuwa ameenda kwa saluni na kusukwa nywele ili kuficha sura yake.

Hata hivyo, wapelelezi waliokuwa wanamuandama waliweza kumkamata alipokuwa anatoroka kwa pikipiki.