MAUAJI KWALE

Kwale: Mwanaume aliyetuhumiwa kuchinja bibiye akamatwa akijaribu kutorokea Tanzania

Hamatton Karisa, 35, anashukiwa kumuua bibiye kwa upanga kisha kuacha mwili kando ya barabara ukiwa umezungukwa na dimbwi la damu na mtoto wa mwaka mmoja mgongoni

Muhtasari

•Inaaminika kuwa Karisa alimchinja bibiye, marehemu Nehema George Karisa, kwa kutumia panga hadi akaaga  baada ya kumuendea kutoka kwa wazazi wake pande za Bamba ambako alikuwa amerudi kuishi kwani wawili hao walikuwa wamezozana

•Mtu mmoja ambaye alimuona mshukiwa akijaribu kuingia Tanzania katika mpaka wa Lunga Lunga aliarifu maafisa wa DCI kupitia mtambo wa simu na wapelelezi katika kituo cha Ganze wakafanya hara kumkamata kabla hajatoweka.

Mshukiwa Hamatton Ismael Karisa
Mshukiwa Hamatton Ismael Karisa
Image: Twitter: dci

Maafisa wa polisi wanazuilia mwanaume mmoja anayetuhumiwa kumuua bibi yake kinyama  mapema mwakani baada ya kumkamata akijaribu kutorokea nchi jirani ya Tanzania.

Hamatton Ismael Karisa,35, alikamatwa siku ya Jumanne katika maeneo ya wa Lunga Lunga alipokuwa anajaribu kuvuka mpaka kuingia Tanzania baada wapelelezi wa DCI kupokea taarifa kutoka kwa mtu aliyemuona akijaribu kutoroka.

Inaaminika kuwa Karisa alimchinja bibiye, marehemu Nehema George Karisa, kwa kutumia panga hadi akaaga  baada ya kumuendea kutoka kwa wazazi wake pande za Bamba ambako alikuwa amerudi kuishi kwani wawili hao walikuwa wamezozana.

"Karisa alifika kwa wazazi wa Nehema ili kusuluhisha matatizo yaliyokumba ndoa yao. Baada ya kujadialiana kwa masaa kadhaa, aliweza kuwashawishi wazazi wa marehemu kuwa warudi nyumbani pamoja na mtoto wao wa mwaka mmoja" ripoti iliyochapishwa na DCI ilisoma.

Watatu hao waliandamana kurudi nyumbani kwao bila ya Nehema kujua  maafa  yaliyokuwa yamemngoja  kwani Karisa alikuwa amepanga njama ya kumuua.

Saa moja tu baada ya safari ya kurudi nyumbani kung'oa nanga, mwili wa Nehema ulipatikana ukiwa umelala kando ya barabara karibu na kituo cha chifu wa Bamba.

Pande ya nyuma ya shingo ya marehemu ilikuwa na majeraha makubwa ya kukatwa kwa panga. Jambo la kusitikisha zaidi ni kuwa mtoto wa mwaka mmoja alipatikana akiwa bado amefungiliwa kwenye mgongo wa mamake na kuzungukwa na dimbwi la damu.

Kufuatia tukio hilo, mshukiwa hakuwahi patikana licha ya juhudi kubwa za wapelelezi kujaribu kumnasa kutoka mafichoni mwake.

Mtu mmoja ambaye alimuona mshukiwa akijaribu kuingia Tanzania katika mpaka wa Lunga Lunga aliarifu maafisa wa DCI kupitia mtambo wa simu na wapelelezi katika kituo cha Ganze wakafanya hara kumkamata kabla hajatoweka.

Mshukiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka siku ya Jumatano.