MAUAJI RONGAI

Polisi aliyetuhumiwa kuua kondakta awachiliwa kwa dhamana ya 800000

Konstebo Okimaru aliamuriwa kutoenda karibu na maeneo ya Ole Kasasi hadi wakati kesi itasizwa na kukamilika.

Muhtasari

•Odunga aliagiza mshukiwa aondolewe kutoka kituo cha polisi cha Muthaiga ambako alikuwa amezuiliwa na kupelekwa katika gereza la Kitengela hadi wakati dhamana italipwa. 

•Mshukiwa pia aliagizwa asijaribu kuingilia washahidi wa upande wa mashtaka kwa namna yoyote ama namna kesi ya upande wa mashtaka itakuwa inaendelea.

Constable Okimaru
Constable Okimaru
Image: george owiti

Polisi aliyekamatwa kwa tuhuma za kumuua kondakta amewachiliwa huru kwa dhamana ya shilingi laki nane.

Konstebo Edwin Oscar Okimaru alifikishwa mbele ya jaji George Odunga katika mahakama kuu ya Machakos siku ya Alhamisi kwa shtaka la kusababisha maafa ya Joshua Mungai mwezi wa Aprili.

Odunga aliagiza mshukiwa aondolewe kutoka kituo cha polisi cha Muthaiga ambako alikuwa amezuiliwa na kupelekwa katika gereza la Kitengela hadi wakati dhamana italipwa. 

Aliamrisha dhamana hiyo kupitishwa na naibu karani wa mahakama kuu ya Machakos.

Okimaru aliamuriwa asipatikane karibu na maeneo ya Ole Kasasi, Ongata Rongai ambapo anadaiwa kushambulia Mungai na marafiki zake wawili hadi wakati kesi itasizwa na kukamilika.

Mshukiwa pia aliagizwa asijaribu kuingilia washahidi wa upande wa mashtaka kwa namna yoyote ama namna kesi ya upande wa mashtaka itakuwa inaendelea.

Aliamuriwa kufika mahakamani kama alivyoagizwa na iwapo atakiuka masharti , dhamana itafutwa na atazuiliwa tena hadi wakati kesi itaamuriwa.

Okimaru alikamatwa tarehe 14 mwezi uliopita baada ya upelezi wa DCI kudhibitisha kuwa alikuwa kwenye eneo la tukio ambapo Mungai na marafiki walishambuliwa.

Ilidaiwa kuwa mnamo tarehe kumi na nane mwezi wa Aprili mida ya saa nne usiku, marehemu Njenga ambaye alikuwa kondakta wa matwana upande wa Ongata Rongai pamoja na marafiki wengine wawili waliotambulishwa kama Njenga na George walikamatwa kwa kukaidi sheria za amri ya kutoka nje.

Watatu hao walishambuliwa na maafisa waliowakamata kisha kufungiwa ndani ya buti ya gari ya kibinafsi na kubebwa hadi kwenye daraja la Tuala ambapo walitupwa.

Mungai alipatwa na msamaria mwema aliyempeleka katika kituo cha afya cha Ongata Rongai alipopewa huduma ya kwanza kisha kupelekwa katika hospitali ya Kenyatta akiwa hali mahututi.

Siku mbili baadae marehemu aliiga dunia akipokea matibabu. Uchunguzi ulibaini kuwa marehemu aliaga kutoka na majereha kifuani. Mungai pia alikuwa amevunjwa mbavu na mifupa kadhaa ishara kuwa alikuwa ameshambuliwa na kunyanyaswa.