Jeshi la anga lafanya ibada ya kuwakumbuka wanajeshi 11 walioaga kufuatia ajali ya ndege

Jeshi la anga limechapisha majina ya 11 ambao waliaga kufuatia ajali hiyo.

Muhtasari

•Ibada ya kuwakumbuka wanajeshi 11 ambao walifariki kufuatia ajali ya ndege wiki iliyopita  ilifanyika siku ya Alhamisi, Julai 1, katika uwanja wa ndege za kijeshi wa Moi.

•Meja Jenerali wa jeshi la anga nchini Kenya, Francis Omondi Ogolla aliomboleza wanajeshi hao  na kusema kuwa walijitolea kuhudumia  jeshi ya anga hadi kifo chao.

Wanajeshi ambao waliaga kufuatia ajali ya ndege wiki iliyopita
Wanajeshi ambao waliaga kufuatia ajali ya ndege wiki iliyopita
Image: Hisani

Ibada ya kuwakumbuka wanajeshi 11 ambao walifariki kufuatia ajali ya ndege wiki iliyopita  ilifanyika siku ya Alhamisi, Julai 1, katika uwanja wa ndege za kijeshi wa Moi.

Meja Jenerali wa jeshi la anga nchini Kenya, Francis Omondi Ogolla aliomboleza wanajeshi hao ambao walihusika kwenye ajali ambayo iliyofanyika maeneo ya Kajiado.

Ogolla alisema kuwa 11 hao walijitolea kuhudumia  jeshi ya anga hadi kifo chao.

"Walitia bidii na walijitolea sana katika kazi yao ya jeshi na kupata heshima kubwa kutoka kwa wakubwa wao, wenzao na hata wadogo wao" Ogolla alisema kupitia ujumbe wa kuchapishwa.

Ogolla alifariji familia za wanajeshi hao na kusema kuwa kifo kimepokonya taifa la Kenya wanajeshi ambao walikuwa wamejitolea, waaminifu na wenye bidii.

"Walikuwa  wamejitolea, walitii amri, walikuwa wachangamfu na ilipendeza kufanya kazi nao. Kifo kimetupokonya wanajeshi ambao wamejitolea, waaminifu, wenye bidii na ambao nyota yao ya usoni iling'aa" Ogolla alisema.

Wanajeshi 23 walikuwa wameabiri ndege aina ya Mi-171e chopper ambayo ilianguka na kulipuka dakika chache tu baada ya kupaa kutoka uwanja wa Moi Airbase upande wa Eastleigh.

Inadaiwa kuwa 12  kati yao walinusuriwa baada ya kuruka wakati ndege hiyo ilikuwa inaanguka  na kukimbizwa hospitalini. Hata hivyo, 11  ambao walikuwa ndani walipoteza maisha yao.

Walionusuriwa walilazwa katika hospitali ya Forces Memorial Hospital. Rais Kenyatta aliwatembelea na kuwatakia afueni.

Jeshi la anga limechapisha majina ya 11 ambao waliaga kufuatia ajali hiyo.

Wanajeshi waliopoteza maisha yao ni Joshua Obare Odera, Tarcisio Wandera Namboka, Noah Wanyonyi Munialo, Ssgt Bob Kipkemoi Aruasa, Ssgt Anthony Simon Kamuti, Ssgt Irene Wanjiku Githinji, Sgt Josphat Muriuki Maingi, Sgt Steve Ombuka Angwenyi, Sgt Stephen Omarian Omale, Cpl Bonface Ogati Mocheche naSpte Thomas Shekeine.