Polisi Nakuru wawinda afisa wa kike anayedaiwa kupiga risasi na kuua polisi mpenziwe

Inatuhumiwa kuwa huenda mauaji yalifuatia mzozo wa kimapenzi.

Muhtasari

•Marehemu alikuwa na majeraha kichwani na damu ilikuwa ikitoka kwenye mapua na maskio. 

Gari la marehemu John Obweno
Gari la marehemu John Obweno
Image: LOISE MACHARIA

Maafisa wa polisi wanamuwinda polisi mmoja wa kike ambaye ni mtuhumiwa mkuu kwenye mauaji ya konstabo wa polisi mjini Nakuru yaliyofanyika siku ya Jumatatu.

Mwili wa Konstabo John Obweno, 28, ulipatikana ndani ya gari lake kwenye maegesho ya gari ya kituo cha polisi cha Kasarani kilicho kaunti ya Nakuru..

Naibu kamishna wa mji wa Nakuru, Joseph Tunoi alisema kuwa Obweno alionekana kwa mara ya mwisho akiwa ameandamana na mpenzi wake koplo Caroline Kangogo ambaye kwa sasa hajulikani aliko.

Inatuhumiwa kuwa huenda mauaji yalifuatia mzozo wa kimapenzi. Mshukiwa alitoroka eneo la tukio punde baada ya kutekeleza hayo

Polisi ambao walifika katika eneo la tukio walishuku kuwa marehemu alipigwa risasi upande wa kulia wa kichwa na akavunja damu hadi kuaga. Walisema kuwa marehemu alikuwa na majeraha kichwani na damu ilikuwa ikitoka kwenye mapua na maskio. 

Injini ya gari  ilikuwa inanguruma bado wakati maafisa wa walifika pale.

Kibweta cha risasi moja cha milimita 9 na chuma kilichotumika kuvunja dirisha ya gari la marehemu ni baadhi ya vitu zilizopatikana katika eneo la tukio.

Polisi wanatia juhudi za kumtafuta mshukiwa na bastola ya Ongweno aina ya Ceska iliyokuwa na risasi 15 ambayo  haikupatikana.

Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika mochari ya Nakuru huku upasuaji wa mwili ukisubiriwa.