Raila apuuzilia mbali 'Bottom up'

Muhtasari

• Raila alisema panafaa pawepo sera za kusaidia wawekezaji wa humu nchini ili kuimarisha biashara zao.

• Alisema mfumo huu wa kutoza kodi unahujumu sana wafanyibiashara wadogo wadogo.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga
Kiongozi wa ODM Raila Odinga

Aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga amekashifu mfumo wa uchumi wa ‘bottom up’ unaopendekezwa na naibu rais  William Ruto akisema kwamba mfumo huo ni wa  Kuwafumba wakenya macho.

Akizungumza katika eneo la Tigoni kaunti ya Kiambu siku ya Alhamisi alipokutana na wafanyibiashara Raila alisema kwamba njia mwafaka ya kuimarisha uchumi wa taifa ni kuimarisha uwekezaji wa humu nchini.

Kinara wa ODM alisema kwamba kama taifa haiwezekani kuimarisha uchumi wa taifa la Kenya kwa kuleta nchini wawekezaji wa kimataifa ambao lengo lao kuu ni kupata faida na kisha kurejesha pesa zao kwa wenye hisa wa kampuni zao.

Raila alisema panafaa pawepo sera za kusaidia wawekezaji wa humu nchini ili kuimarisha biashara zao.

Waziri mkuu wa zamani alikosoa sera ya utoaji kodi nchini akisema kwamba inawagandamiza wawekezaji wa humu nchini hatua ambayo imepelekea kusambaratika kwa biashara nyingi nchini.

Alisema mfumo huu wa kutoza kodi unahujumu sana wafanyibiashara wadogo wadogo.

“Lazima kuwe na mpango madhubuti, uliofikiriwa vizuri wa kujenga uchumi. Nchi yetu haitaweza kutegemea ahadi zilizojengwa kwa mifano ya uchumi ambayo hajajaribiwa na ambayo nguzo zake ni utapeli. Mawazo haya ni takataka” Raila alisema.

Raila alikariri msimamo wake wa kudhibiti ushuru na kodi wanazotozwa wawekezaji akisema kwamba zimekuwa kizingiti kikubwa katika sekta ya uwekezaji.

Naibu rais Wiliam Ruto na wandani wake wamekuwa wakipigia debe mfumo wa kuboresha uchumi unaolenga kukuza uchumi wa taifa kuanzia kwa mtu wa chini ‘Bottom up’ mfumo ambao Raila na wandani wake wamesema hauwezi kutekelezwa bali ni wa kuwahadaa tu wakenya.