Polisi 2 wakamatwa kwa jaribio la wizi wa mabavu

Muhtasari

Katika harakati za kutoroka, afisa mmoja aliangusha simu yake ya mawasiliano ya polisi, ambayo ilipatikana na polisi waliokuwa katika doria.

Uchunguzi wa awali ulifichua kwamba kifaa hicho cha mawasiliano kilikuwa kimepewa Soita, ambaye ndiye msimamizi wa kituo cha Doria cha Lower Kabete.

Pingu
Image: Radio Jambo

Maafisa wawili wa polisi wamekamatwa kwa tuhuma za jaribio la wizi wa mabavu katika eneo la Kioko, Dagoretti.

Kulingana na Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, maafisa hao waliotambuliwa kama Inspekta Evans Soita na Konstebo John Kemboi waliingia kwenye duka la Stephen Kamotho huko Dagoretti saa tano asubuhi siku ya Jumatano na makabiliano yakaanza.

Maafisa hao wanaohudumu katika kituo cha Polisi cha Spring Valley kisha walimtishia mwenye duka kwa bunduki na kujaribu kumuweka pingu.

 Kamotho kisha alipiga kamza na wananchi wakaja kumwokoa kutoka kwa maafisa hao.

"Walipoona wamezingirwa na wananchi, maafisa hao waliamua kutoroka kwa kupiga risasi moja angani ili kuogofya umati huo uliokuwa na hamaki," DCI alisema.

Wakati wa patashika hiyo, Kamotho alijeruhiwa mkono wake wa kushoto na tumbo na akukimbizwa hospitali ya Nile kupata matibabu.

Katika harakati za kutoroka, afisa mmoja - Inspekta Soita alipoteza simu yake ya mawasiliano ya polisi, ambayo ilipatikana na polisi waliokuwa katika doria ambao walikuwa wamewasili kudhibiti hali.

"Maafisa wa polisi waliokuwa doria huko Kikuyu, walikimbilia eneo la tukio na kufanikiwa kutuliza hali na kuchukuwa kifaa muhimu cha mawasiliano cha polisi."

Uchunguzi wa awali ulifichua kwamba kifaa hicho cha mawasiliano kilikuwa kimepewa Soita, ambaye ndiye msimamizi wa kituo cha Doria cha Lower Kabete.

Maafisa hao wawili walikamatwa, wakapokonywa silaha na kuwekwa chini ya ulinzi katika kituo cha polisi cha Gigiri.

Watafikishwa mahakamani.