Mfanyibiashara awasilisha ombi la kuondolewa kwa DPP Haji

Muhtasari

• Francis Njeru anadai kuwa DPP amesimamia visivyo kesi yake ambapo kuna mzozo wa mali baina yake na kampuni ya China Road Bridge Corporation, na ARJ Capital.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji
DPP Norrdin Haji Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji
Image: Maktaba

Mfanyabiashara wa mjini Nairobi amewasilisha ombi la pili kwa Tume ya Utumishi wa Umma kutaka kuondolewa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji afisini kwa utovu wa nidhamu.

Ombi la kwanza liliwasilishwa na dada wa marehemu Tob Cohen, Gabriel Van Straten akimtuhumu DPP kwa kusimamia vibaya kesi ya mauaji ya kaka yake.

Francis Njeru anadai kuwa DPP amesimamia visivyo kesi yake ambapo kuna mzozo wa mali baina yake na kampuni ya China Road Bridge Corporation, na ARJ Capital.

Mali inayozungumziwa iko kando ya barabara ya Mombasa katika eneo la Kyangombe huko Embakasi na Njeru imedai wake.

Njeru ameiambia PSC kwamba baada ya uchunguzi wakurugenzi wa ARJ Capital Ahmed Rashid Jibril na Farah Ali Mohamed ambao wanadaiwa wanahusiana na Haji walishtakiwa mnamo Januari 2020 kwa kula njama ya ulaghai, kutengeneza hati ya uwongo, na kupata usajili wa ardhi kwa udanganyifu.

Hata hivyo, mwezi Machi 2, 2020, Njeru anadai kuwa DPP alitoa ombi la kuondoa kesi hiyo kortini lakini wakili wake alipinga ombi hilo na hakimu pia alikataa.

Korti iliamua kwamba ombi  hilo linapaswa kusikilizwa na kuamuliwa kwa ukamilifu kwani uchunguzi ulikuwa umefafanuliwa sana.

Kupitia kwa Wakili Danstan Omari na Cliff Ombeta, Njeru anadai kwamba DPP alikwenda  Mahakama Kuu kwa nia ya kufuta mashtaka mbele ya Jaji Daniel Ogembo lakini jaji alikataa kuondoa kesi hiyo.

Inadaiwa kwamba walirudi mahakamani na mwendesha mashtaka alihimiza korti iepuke jaribu la kuingilia uhuru wa DPP hata akidokeza kwamba Njeru pia anaweza kuwasilisha kesi ya kibinafsi ikiwa azimio lake lilikuwa lazima kesi hiyo ikamilishwe.

Korti iliruhusu ombi la kujiondoa na ikampa mwombaji fursa ya kufuata mashtaka ya kibinafsi na ikampa ruhusa ya kufanya hivyo.