Mikasa ya moto shuleni, mbunge ataka mashauriano na wanafunzi

Muhtasari

• Odhiambo alibainisha kuwa vijana wanapaswa kuwaheshimu wakubwa wao, wazazi na walimu ili wafanikiwe maishani.

• Alisema kuwa wanafunzi waliokuwa wakisababisha machafuko na uharibifu kwa kuchoma shule zao hawana maadili na tabia nzuri na kudharau kanuni za jamii.

Mwakilishi wa wanawake wa Migori Pamela Odhiambo
Mwakilishi wa wanawake wa Migori Pamela Odhiambo
Image: Pamela Odhiambo twitter

Ushauri umetolewa kufanyika kwa mashauriano ya kina kati ya Bodi simamizi za Shule (BOM), wazazi na Wizara ya Elimu kushughulikia suala ya machafuko shuleni.

Mwakilishi wa Wanawake wa Migori Pamela Odhiambo ametaka mazungumzo hayo kufanyika haraka iwezekanavyo. Akizungumza mwishoni mwa wiki Odhiambo alibainisha kuwa ni jambo la kuhuzunisha kuona wanafunzi wakichoma shule, taasisi ambazo zinazopaswa kuwafinyanga kuwa viongozi wanaowajibika siku zijazo.

Mwakilishi huyo wa wanawake alisema wasimamizi wa shule wanapaswa kujitahidi kila wakati kujua kile ambacho wanafunzi walitaka badala ya kile wanachohitaji.

“Wakati mwingine si vibaya kuwasikiliza wanafunzi kuhusu masuala mbalimbali ambayo yanaweza kuwaathiri. Ni bora kujadiliana na wanafunzi hawa na kuwa na kuweka mikakati ya kuzuia badala ya kuwapuuza na kujuta baadaye, "alisema.

Hata hivyo, Odhiambo alibainisha kuwa vijana wanapaswa kuwaheshimu wakubwa wao, wazazi na walimu ili wafanikiwe maishani.

Alisema kuwa wanafunzi waliokuwa wakisababisha machafuko na uharibifu kwa kuchoma shule zao hawana maadili na tabia nzuri na kudharau kanuni za jamii.

"Wazazi, BOM na wananchi wamechukua miaka mingi kujenga shule kote nchini na inatia uchungu kuona wanafunzi wahuni wakichoma kwa dakika chache," Odhiambo alilalamika.

Mbunge huyo alisema haikuwa haki kwa wanafunzi hao kuchoma mabweni yao na bado kizazi kijacho kinatakiwa kutumia taasisi hizo hizo.