Mchungaji mla kondoo wake! Mhubiri asakwa kwa kunajisi msichana wa kidato cha tatu kisha kutoweka Makueni

Muhtasari

‚ÄĘKimeu ambaye anahudumu katika kanisa ya AIC Kalebwani alimuona mhasiriwa akitoka shuleni na akajitolea kumbeba kwa gari yake.

Roman style cassock
Roman style cassock
Image: PACEPRENUER.COM

Wapelelezi katika kaunti ya Makueni wanamsaka kasisi mmoja aliyebaka msichana wa miaka 18 kisha kumpa onyo asiambie mtu yeyote kuhusu yaliyotendeka.

Mhubiri huyo aliyetambulishwa kama mchungaji Daniel Kimeu anaripotiwa kumbaka mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu alipokuwa anatoka shuleni mnamo Oktoba 19.

Kulingana na DCI, Kimeu ambaye anahudumu katika kanisa ya AIC Kalebwani alimuona mhasiriwa akitoka shuleni na akajitolea kumbeba kwa gari yake.

Msichana yule alisimulia kwa mwalimu wake kuwa baada ya kusafiri umbali wa kilomita chache Kimeu alisimamisha gari lake katika eneo lililokuwa limejificha na akaanza kumnajisi.

Mhasiriwa alisema Kimeu alikuwa amemuona katika soko ya Kikuswi  akitembea kuelekea nyumbani, akasimamisha gari lake na kumsihi aingie.

Kwa kuwa msichana yule alikuwa na imani kubwa kwamba mtumishi yule wa Mungu hangekuwa na nia mbaya juu yake aliridhishwa na ukarimu wake na kuingia ndani ya gari bila kujua hatari iliyokuwa imemkondolea macho.

Baada ya kutekeleza unyama huo mchungaji Kimeu anadaiwa kuenda mafichoni asijulikane aliko hadi kufikia sasa.

Maafisa wa DCI wameomba yeyote aliye na habari ambazo zaweza saidia kukamatwa kwa Kimeu asisite kupiga ripoti kwa polisi ili mhalifu aweze kukamatwa na kushtakiwa.