Wazazi walalamikia uuzaji wa pombe karibu na shule Kisii

Muhtasari

• Wazazi hao walitoa wito kwa mamlaka kushughulikia wahalifu ambao walisema wamekuwa wakitekeleza uovu huo licha ya kukamatwa mara kadhaa na polisi.     

• Wanafunzi 27 wa shule hiyo kwa sasa wamefukuzwa kwa kupatikana na chang’aa ambayo walipata kwa muuzaji aliyekaribu na shule.   

Image: MAKTABA

Wazazi wa shule ya upili ya St. Joseph's Nyabigena katika Kaunti Ndogo ya Gucha Kusini, Kaunti ya Kisii wamegadhabishwa na madai kuwa wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakipata pombe haramu kwa urahisi wakiwa shuleni wakisema inaharibu maisha ya baadaye ya watoto wao.            

Wakihutubia wanahabari mjini Tabaka siku ya Jumatatu, wazazi hao walitoa wito kwa mamlaka kushughulikia wahalifu ambao walisema wamekuwa wakitekeleza uovu huo licha ya kukamatwa mara kadhaa na polisi.             

Mwanachama wa Bodi ya Usimamizi wa shule Edwin Nyang’au, Mwenyekiti wa muungano wa Wamiliki wa baa na Hoteli Eric Matoke na wawakilishi wa wazazi Bethsheba Abuya na Hesbon Nyakundi walitaka kukutana na Naibu Kamishna wa Kaunti hiyo Edonga Nanok wakisema baadhi ya washukiwa walikuwa majirani wa shule hiyo na kujulikana sana na jamii.  

           Nyang’au alibainisha kuwa wanafunzi 27 wa shule hiyo kwa sasa wamefukuzwa kwa kupatikana na chang’aa ambayo walipata kwa muuzaji aliyekaribu na shule.             

"Shughuli kama hizo zimesababisha kuchomwa kwa bweni katika shule hiyo hapo awali," alilalamika Nyang’au.     

      

Abuya alisimulia jinsi watoto wa shule wanavyoficha pesa katika sehemu fiche kando ua la shule, ambapo wafanyabiashara huzichukuwa na kisha kusambaza pombe inayolingana na kiasi cha pesa.            

Matoke ambaye pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Wazazi wa shule hiyo alishangaa ni kwa nini uuzaji wa mvinyo na pombe kali uliruhusiwa karibu na taasisi kama vile shule na hospitali, akiongeza kuwa biashara hizo zisizo na leseni huchanganya vileo halisi na haramu.             Nyakundi sasa anataka utawala kukomesha biashara hito akisema mustakabali wa watoto wao unatishiwa.            

Hata hivyo naibu kamishna wa kaunti alibainisha kuwa serikali imejitolea kuwalinda wanafunzi na hapo awali maafisa wa usalama waliwakamata baadhi ya wahusika na kuwafikisha mahakamani ambapo walilipa faini ya kati ya shilingi 8,000 na shilingi 12,000.             

Nanok alitoa wito kwa jamii kujitolea kutoa habari kuhusu vitendo vyovyote vya uhalifu, huku akiahidi kushirikisha mahakama kwa adhabu kali ili kukomesha pombe haramu katika Kaunti Ndogo ya Gucha.