Serikali kuimarisha elimu ya watoto wenye mahitaji maalum

Muhtasari

• Wizara ya Elimu inatarajia kufanyia marekebisho Vituo vya Tathmini na Rasilimali za Elimu (EARCS) kwa nia ya kuimarisha uwezo wake wa kutathmini asili na viwango vya ulemavu miongoni mwa watoto.

• Tathmini hiyo itaiwezesha serikali kuamua juu ya hatua zinazohitajika ili kupunguza ulemavu na kuwaweka watoto katika taasisi zinazofaa za Elimu.

Wanafunzi wa Shule Maalum ya Nyaburi. Picha: KNA
Wanafunzi wa Shule Maalum ya Nyaburi. Picha: KNA

Wizara ya Elimu inatarajia kufanyia marekebisho Vituo vya Tathmini na Rasilimali za Elimu (EARCS) kwa nia ya kuimarisha uwezo wake wa kutathmini asili na viwango vya ulemavu miongoni mwa watoto.

Tathmini hiyo itaiwezesha serikali kuamua juu ya hatua zinazohitajika ili kupunguza ulemavu na kuwaweka watoto katika taasisi zinazofaa za Elimu.

Ufichuzi huo ulitolewa na naibu waziri wa elimu, Bi Mumina Bonaya wakati wa hafla ya kufunga Kongamano la latu la Kitaifa kuhusu Elimu Maalum katika Taasisi hiyo jijini Nairobi Alhamisi jioni.

Alisema maguezi mapya katika taasisi ya EARCS yatahakikisha uwekaji, ufikiaji, usawa, ubora, umuhimu, mpito na ukamilishaji wa viwango vyote vya elimu kwa watoto wote katika ngazi zote kwa 100% kuambatana na Mtaala wa CBC.

Mumina alisema wazazi wanapaswa kuwasilisha watoto wao wenye ulemavu wa aina mbalimbali kwa EARCS ambapo serikali inaweza kufanya tathmini ya ulemavu na kuwaweka watoto katika taasisi za elimu zitakazokuza uwezo na vipaji vyao.

Alieleza wasiwasi wake kuwa baadhi ya wazazi wanawaficha watoto hivyo kuwanyima fursa ya kukuza uwezo na vipaji vyao vya kuzaliwa.

Alisema sera ya serikali kuhusu Elimu inalenga kumsomesha kila mtoto bila kumwacha mtoto yeyote.

Alisema CBC ilitoa utofauti ikilenga uwezo wa kila mtoto bila kujali maumbile yake.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dk.Norman Kiogora alisema Elimu ya watoto wenye mahitaji Maalum haikuthaminiwa kwa urahisi.

Alisema watoto hao walikuwa na matatizo ya kihisia na kujifunza ambayo walimu walihusisha na utukutu.

Alipendekeza taasisi za mafunzo kwa walimu zifundishe programu za Elimu yenye mahitaji maalum ili wawe na ujuzi na ufahamu wa kushughulikia watoto wenye mahitaji maalum.