Watu 20 wafariki, 10 waokolewa baada ya basi kuzama mtoni Kitui

Basi hilo lilikuwa limebeba abiria waliokuwa wanaenda kuhudhuria harusi.

Muhtasari

•Inahofiwa huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka uokoaji unapoendelea kwani idadi halisi ya abiria waliokuwemo bado haijathibitishwa.

Basi lililozama
Basi lililozama
Image: HISANI

Watu 18 wamethibitishwa kufariki huku wengine 10 wakiokolewa baada ya basi kuzama katika mto wa Enziu ulio eneo la Mwingi kaunti ya Kitui.

Kamanda wa polisi katika eneo hilo Joseph Yakan amesema basi hilo  la shule ya Sekondari ya Mwingi Seminary lilikuwa limebeba abiria waliokuwa wanaenda kuhudhuria harusi.

Tukio hilo linaripotiwa kutokea mwendo wa saa tano asubuhi ya Jumamosi katika kijiji cha Ngue, wadi ya Nuu.

Basi hilo lilikuwa limebeba zaidi ya  abiria 30 ambao wanasemekana kuwa wanakwaya kutoka kanisa la katoliki la Mwingi.

Katika video iliyoonekana na Radio Jambo, basi hilo lilikuwa linajaribu kuvuka daraja lililokuwa limefurika  maji wakati mikondo ya maji yenye nguvu ililibeba na kulizamisha ndani ya mto.

Kilio na nduru kubwa  kutoka kwa wanakijiji ambao walishuhudia zilitanda hewani katika eneo la tukio punde baada ya ajali hiyo ya kusikitisha kutokea. Magari mengine yalionekana kuhofia kuvuka daraja lile.

Yakan amesema kwa sasa basi hilo bado limezama kwenye matope huku akiongeza kuwa juhudi za uokoaji zinaendelea.

Inahofiwa huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka uokoaji unapoendelea kwani idadi halisi ya abiria waliokuwemo bado haijathibitishwa.

Mengi yanafuata...