Rais Uhuru, DP Ruto, Raila waomboleza waliofariki katika ajali mbaya iliyotokea Mwingi na kufariji familia zao

Muhtasari

•Kufikia kusimamishwa kwa shughuli ya uokoaji jioni ya Jumamosi, watu 24 walithibitishwa kufariki huku wengine 12 wakiokolewa.

•Kufuatia habari hizo za kuhuzunisha ambazo sasa zimeenea kote ulimwenguni, maelfu ya Wakenya wameendelea kuwaomboleza wahasiriwa walioangamia huku wakifariji familia na wapendwa wao.

Shughuli ya uokoaji yaendelea
Shughuli ya uokoaji yaendelea
Image: HISANI

Hali ya majonzi ilitanda kote nchini siku ya Jumamosi baada ya habari kuhusu ajali mbaya iliyotokea katika eneo la Mwingi ya kati, kaunti ya Kitui kugonga vichwa vya habari.

Basi iliyokuwa imebeba abiria zaidi ya 30 waliokuwa wanaenda kuhudhuria harusi liliwezwa na mikondo ya maji yenye nguvu, likapinduka na kuzama ndani ya mto wa Enziu wakati lilijaribu kuvuka daraja lililokuwa limefurika  maji.

Abiria waliokuwa ndani ya basi hilo la shule ya Sekondari ya Mwingi Seminary wanaripotiwa kuwa waumini kutoka kanisa ya katoliki ya Mwingi ikiwemo watoto.

Kufikia kusimamishwa kwa shughuli ya uokoaji jioni ya Jumamosi, watu 24 walithibitishwa kufariki huku wengine 12 wakiokolewa.

Kufuatia habari hizo za kuhuzunisha ambazo sasa zimeenea kote ulimwenguni, maelfu ya Wakenya wameendelea kuwaomboleza wahasiriwa walioangamia huku wakifariji familia na wapendwa wao.

Rais Uhuru Kenyatta amefariji familia za wahasiriwa ambao walipoteza maisha yao kufuatia msiba ule  huku akiwatakia manusura wanaopokea matibabu kupona kwa haraka.

Kupitia kwa msemaji wa ikulu Kanze Dena, rais pia ametahadharisha Wakenya dhidi ya kujaribu kuvuka mito iliyofurika katika msimu huu wa mvua.

"Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala zake za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao katika mkasa wa kusikitisha huko Mwingi, Kaunti ya Kitui wakati basi walimokuwa wakisafiria kutumbukia katika mto Enziu jana.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais anawatakia ahueni ya haraka wale waliojeruhiwa katika tukio hilo la kusikitisha. Kwa mara nyingine, Rais anapenda kuwakumbusha Wakenya kote nchini kutii ushauri wa Serikali dhidi ya kujaribu kuvuka mito iliyojaa maji hasa wakati wa msimu wa mvua.

Taarifa zaidi kuhusu tukio hilo la kusikitisha na hatua ambazo Serikali inachukua ili kuzuia maafa kama haya yasijirudie zitatolewa kwa wakati ufaao." Dena aliandika.

Kinara wa ODM Raila Odinga pia alituma risala zake za rambirambi kwa familia na wapendwa wa walioangamia na kuwaombea nguvu ya kupambana na majonzi  yaliyowapata ghafla huku akitakia marehemu mapumziko yenye amani.

"Sala na rambirambi zangu ziende kwa familia za tuliowapoteza mchana wa leo wakati basi lililokuwa limebeba Kwaya ya Kanisa Katoliki la Mwingi lilipotumbukia mto Enziu. Mungu patie walioathirika nguvu na azilaze roho za marehemu mahala pema peponi." Raila alisema.

Naibu rais William Ruto alifariji familia za waliopoteza maisha yao huku akitakia walionusurika kupona kwa haraka.

Vile vile alihimiza waendesha magari kuwa makini zaidi haswa katika msimu huu wa mvua kubwa ambayo inanyesha kote nchini

"Mawazo yetu yako pamoja na familia, wapendwa na marafiki wa wale walioangamia kwenye ajali mbaya eneo la Mwingi, Kaunti ya Kitui. Tunatuma maombi yetu na kutakia kupona kwa haraka kwa walionusurika. Tunawaomba madereva wa magari kuwa waangalifu zaidi hasa wakati huu tunapokabiliwa na mvua kubwa kote nchini" Ruto alisema.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye pia ametoka eneo hilo alifariji na kuombea familia za walioangamia nguvu ya kupambana na majonzi huku akitakia walionusurika kupona kwa haraka.

"Moyo wangu unaenda kwa familia za waumini wa Kanisa Katoliki la Mwingi waliopoteza maisha katika ajali mbaya ya mto Enziu, Mwingi, Kaunti ya Kitui. Mawazo yangu pia yako kwa walionusurika na familia zao. Nawaombea wote waliolazwa wapone haraka. Pia namuomba Mwenyezi Mungu awafariji wale wote ambao huzuni yao kwa wakati huu haina kipimo." Alisema Kalonzo.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko alikosoa hatua ya dereva aliyekuwa anaendesha basi lile kuchukua hatari ya kulivukisha kwa daraja lililofurika huku akiombe roho za waliofariki amani.