Polisi waliojihami vikali wavamia afisi za bwenyenye Jimi Wanjigi zilizo Westlands

Muhtasari

•Afisi hizo zilizo katika mtaa wa Westlands ni kituo cha Kampeni cha Wanjigi ambaye anamezea mate kiti cha urais kwa tiketi ya ODM.

Maafisa wa polisi waliojihami katika afisi za mfanyabiashara Jimi Wanjigi katika Westland.
Maafisa wa polisi waliojihami katika afisi za mfanyabiashara Jimi Wanjigi katika Westland.
Image: HISANI

Usiku wa Jumatatu kikosi cha polisi waliokuwa wamejihami vikali kilivamia afisi za mfanyibiashara na mwanasiasa mashuhuri Jimi Wanjigi zilizo katika eneo la Westands.

Picha za CCTV za uvamizi huo zilithibitisha kuwa ulifanyika mwendo wa saa tatu unusu usiku  na kuendelea hadi saa nne unusu.

Mchekeshaji Eric Omondi ambaye alikuwa anashiriki mkutano na Wanjigi ndani ya afisi hizo alisema maafisa hao walikuwa kutoka kikosi cha Flying Squad.

"Kinachoendelea kwa sasa nje ya afisi zetu za kampeni ya Jimi Wanjigi..Flying Squad wako kwa lango na sisi tuko kwa mkutano ndani" Omondi alisema na kuambatanisha ujumbe wake na picha za CCTV zilizokuwa zinaonyesha matukio ya usiku huo.

Wakili wa Wanjigi, Willis Otieno alithibitisha kuhusu tukio hilo.

Afisi hizo zilizo katika mtaa wa Westlands ni kituo cha Kampeni cha Wanjigi ambaye anamezea mate kiti cha urais kwa tiketi ya ODM.

Inaripotiwa kwamba bwenyenye huyo alikuwa ndani ya afisi zile pamoja na mwanawe wakati wa uvamizi huo.

Uvamizi huo umeibua hisia tofauti huku baadhi ya mawakili na wanasiasa wakihusisha tukio hilo na siasa zinazoendelea.