IEBC yaongeza muda wa kuwasilisha majina ya wagombea wa urais na ugavana

Muhtasari

• Mkutano huo uliafiki kuongeza muda wa vyama vya kisiasa kuwasilisha majina ya wagombeaji wao kwa wadhifa wa urais na nyadhifa za ugavana hadi Mei 16.

• Miungano ya Azimio na Kenya kwanza ilikuwa imepinga makataa ya IEBC kuwa majina hayo yawasilishwe wiki hii na kuomba muda zaidi.

• Chebukati alivishauri vyama vya kisiasa kuhakikisha kuwa orodha zao za uteuzi zinatimiza matakwa ya usawa wa jinsia.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati

Tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imelazimika kubadili msimamo wake wa awali kuhusu makataa ya kuwasilisha majina wagombea wenza kwa wanaowania urais.

Akizungumza baada ya mkutano na vyama vya siku ya Jumanne mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema kwamba waliafikiana kuongeza muda wa kuwasilisha majina ya wagombeaji wenza kwa nafasi za ugava na urais.

Mkutano huo uliafiki kuongeza muda wa vyama vya kisiasa kuwasilisha majina ya wagombeaji wao kwa wadhifa wa urais na nyadhifa za ugavana hadi Mei 16.

Miungano ya Azimio na Kenya kwanza ilikuwa imepinga makataa ya IEBC kuwa majina hayo yawasilishwe wiki hii na kuomba muda zaidi.

Tume ya uchaguzi ilisema kwamba baada ya majina yao kufikia tume yatawasilishwa kwa idara za sura ya sita ili yapigwe msasa kabla ya kuandaliwa kwa mkutano wa wagombeaji mnamo Mei 23.

Chebukati alisema kwamba katika mkutano wa Jumanne walikubaliana kwamba tarehe ya kuwasilisha majina ya wagombeaji kwa nafasi nne za uchaguzi, mbunge, mwakilishi wadi, mwakilishi wa kike na seneta zitasalia Aprili 28.

Hii inamaanisha kuwa vyama vyote vya kisiasa pamoja na wagombeaji huru wana hadi Alhamisi kuwasilisha majina ya wagombeaji kwa tume ya uchaguzi.

Mwenyekiti huyo wa IEBC alisema kwamba sababu ya kutaka majina ya wagombea wa nyadhifa hizo nne kuwasilishwa Aprili 28, ni kuipa tume hiyo muda wa kutosha kuwasilisha majina hayo kwa idara husika za maadili kuambatana na sura ya sita ya katiba ili wagombeaji wote wapingwe msasa.

Chebukati alivishauri vyama vya kisiasa kuhakikisha kuwa orodha zao za uteuzi zinatimiza matakwa ya usawa wa jinsia.