IEBC yaitisha mkutano wa dharura kujadli suala la wagombea wenza

Muhtasari

• Iebc iliamua kuitisha mkutano huo baada ya miungano yote miwili Azimio na Kenya Kwanza kupinga makataa ya Alhamisi.

IEBC/Twitter
IEBC/Twitter
Image: Wafula Chebukati

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Wafula Chebukati ameitisha mkutano wa dharura siku ya Jumanne kujadili makataa ya mgombea mwenza.

Iebc iliamua kuitisha mkutano huo baada ya miungano yote miwili Azimio na Kenya Kwanza kupinga makataa ya Alhamisi.

"Tumewaomba maafisa wanaoongoza campeini za urais za wagombeaji wote waje kwenye mkutano ili tukubaliane kuhusu suala hili," kamishna mmoja alisema.

Mkutano huo ulijiri huku muungano wa Azimio ukijadili uwezekano wa kuwasilisha kesi ya kutaka kubatilisha makataa ya IEBC kuhusu uteuzi wa mgombea mwenza.

Upande wa Naibu Rais William Ruto pia unashauriana kuhusu jinsi ya kusonga mbele iwapo IBEC itasisitiza kwamba mgombea mwenza lazima atajwa kabla ya Alhamisi.

Timu zote mbili za Ruto na Raila zilikuwa zimepinga makataa ya Aprili 28 na kutaka IEBC kupokea majina hayo kati ya Mei 29 na Juni 6.

Hata hivyo, katika barua siku ya Jumapili, Chebukati alisisitiza kuwa wanaowania urais wana hadi mwisho wa Alhamisi kuwasilisha majina hayo.

Msimamo mkali wa IEBC unasemekana kuzua tumbo joto katika mrengo wa Raila kwani na ikaamuliwa kwamba lazima kinara huyo wa ODM afupishe safari yake ya Marekani.

"Hili ni suala ambalo mgombeaji urais lazima ajitokeze kibinafsi, si kazi zinazoweza kukabidhiwa kwa sababu jina hilo linapowasilishwa ni la lazima," mwanasiasa wa ngazi ya juu katika kikosi cha kampeini cha Raila alisema.

 

Raila alipangiwa kusalia Amerika hadi Ijumaa kama sehemu ya shughuli zake za kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia kabla ya uchaguzi.

 

Hata hivyo, msimamo wa IEBC alivruga mipango ya Raila.

 

Sekretarieti ya kampeni ya urais ya Raila ilithibitisha kuwa amekatiza safari yake lakini ikataja programu ya mazishi ya Rais mstaafu Mwai Kibaki kuwa sababu pekee.

 

"Kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga atakatisha safari yake ya Marekani na kurejea nyumbani Jumatano kabla ya mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa Rais Mwai Kibaki," taarifa iliyotiwa saini na Denis Onsarigo ilieleza.