Wasiwasi huku watu 10 wakifariki kwa kujitoa uhai wikendi

Polisi wanashughulikia takriban visa 10 vya kujitoa uhai ambazo ziliripotiwa wikendi pekee

Muhtasari

•Matukio hayo yaliripotiwa katika maeneo tofauti na yamehusishwa na masuala tofauti ndani ya familia.

•Visa vya watu kujiua vimeongezeka mwaka huu, na viongozi wanashuku kuwa hali hiyo kuwa imechangiwa na msongo wa mawazo.

Kamba ya kujiua
Kamba ya kujiua
Image: Image: Courtesy

Polisi wanashughulikia takriban visa 10 vya kujitoa uhai ambazo ziliripotiwa wikendi pekee.

Matukio hayo yaliripotiwa katika maeneo tofauti na yamehusishwa na masuala tofauti ndani ya familia.

Polisi wanasema kumekuwa na ongezeko la visa vya watu kujitoa uhai nchini huku takriban kesi mbili zikiripotiwa kila siku.

Tukio la kwanza liliripotiwa huko Kayole, Nairobi, ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 27 alifariki baada ya kudaiwa kudondoka kutoka orofa ya nne ya ploti anayoishi.

Hii ilikuwa baada ya kuchelewa kufika nyumbani na kukuta familia yake imelala.

Majirani waliambia polisi kuwa mtu huyo alianguka kutoka kwa reli za jengo hilo na kuanguka chini. Alikufa papo hapo.

Mwili mwingine wa mwanamume uliopatikana ukining’inia kwenye mti eneo la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu mnamo Julai 30.

Polisi walisema maafisa walikuwa wakishika doria eneo la Acre Tano walipokutana na mwili huo kwenye mti Jumamosi mchana.

Huko Migori, mwili wa Geoffrey Odhiambo ulipatikana ukining'inia ndani ya nyumba yake baada ya kudaiwa kujitoa uhai.

Polisi walisema waliarifiwa kuwa Mary Wairimu mwenye umri wa miaka 85 alifariki katika nyumba yake eneo la Kiratina kwa kujitoa uhai. Familia iliambia polisi kuwa alikuwa akikaa peke yake na alikuwa na shida za kiakili.

Polisi walisema katika eneo la Eregi, Kakamega, James Lirubi, 55, alifariki kwa kujinyonga nyumbani kwake huku katika eneo la Matungu, Vivian Warire mwenye umri wa miaka 21 akifariki kwa kujitoa uhai nyumbani kwake. Alikuwa mjamzito.

Kulingana na polisi, mwanafunzi wa udaktari alifariki kwa kujinyonga katika chumba chake eneo la Nzambani, Seku, Kaunti ya Kitui. Mwili wa Brian Kipkoech ulipatikana katika chumba chake muda mrefu baada ya tukio hilo kutokea.

Na katika eneo la Sultan Hamud, Kaunti ya Makueni, mwili wa Philip Mutuku, 39, ulipatikana ukining’inia juu ya mti.

Huko Kieni, Nyeri, Wanguku Kariuki, 52, alifariki kwa kujinyonga akiwa Shauri Moyo, Joseph Kiguta mwenye umri wa miaka 38 alipatikana nyumbani kwake baada ya kudaiwa kujitoa uhai mnamo Julai 31.

Polisi walisema miili hiyo ilihamishwa hadi kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti katika maeneo husika kabla ya uchunguzi wa maiti kufanyika.

Visa vya watu kujiua vimeongezeka mwaka huu, na viongozi wanashuku kuwa hali hiyo kuwa imechangiwa na msongo wa mawazo.

Polisi walishughulikia kesi 499 mwaka wa 2019 na 575 mwaka wa 2020. Takriban watu 313 wanaripotiwa kujiua kati ya Januari na Julai 2021.

Wengi wa wahasiriwa walikuwa wanaume, ripoti za polisi zinasema.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema visa hivyo vinachangiwa na ukosefu wa ajira, kuvunjika kwa mahusiano au kifo, kushindwa kitaaluma au shinikizo, matatizo ya kisheria, matatizo ya kifedha, uonevu, majaribio ya awali ya kujiua, historia ya kujiua katika familia, ulevi na madawa ya kulevya, unyogovu na ugonjwa wa bipolar. 

Ulimwenguni kote, karibu watu 800,000 hufa kwa kujiua kila mwaka huku takriban asilimia 78 ya visa vikitokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati. 

Kenya inashika nafasi ya 114 kati ya nchi 175 zilizo na viwango vya juu vya kujiua. Kikosi kazi kuhusu afya ya akili kilichoanzishwa Kenya kina mzigo mkubwa wa magonjwa ya akili kutokana na afya mbaya, ulemavu wa kisaikolojia na vifo vya mapema na mapungufu makubwa katika kupata huduma. 

Timu hiyo iligundua kuwa idadi kubwa ya watu nchini Kenya huhusisha afya ya akili na ugonjwa wa akili na masimulizi mabaya yanayopelekea kuzingatia kwa chini umuhimu na manufaa ya afya ya akili na ustawi. 

Timu hiyo pia ilipendekeza ugonjwa wa akili utangazwe kuwa dharura ya kitaifa ya idadi ya janga, ili kuweka kipaumbele cha afya ya akili kama ajenda ya afya ya umma na kijamii na kiuchumi.

 Ilipendekeza kwamba afya ya akili itolewe kwa ufadhili wa kutosha kulingana na utendaji bora wa kimataifa Nchini Kenya, inakadiriwa kuwa mtu mmoja kati ya 10 ana tatizo la kawaida la akili. 

Idadi hiyo huongezeka hadi mtu mmoja kati ya kila watu wanne kati ya wagonjwa wanaohudhuria huduma za kawaida za wagonjwa wa nje.