DP Gachagua amshambulia DCI na kumtaka kuacha kuhangaisha viongozi

"Tumeambia DCI kurudi katika Barabara ya Kiambu na kusubiri uhalifu kuripotiwa huko."

Muhtasari

•Gachagua vile vile alimsuta DCI kwa madai ya kutuma maafisa wa vyeo vya chini kuwakamata viongozi wa ngazi za juu waliochaguliwa.

Naibu Rais Rigathi Gachagua ameendeleza mashambulizi yake dhidi ya idara mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI). 

Gachagua alikuwa akizungumza siku ya Alhamisi katika ufunguzi wa warsha ya mafunzo kwa magavana wapya mjini Mombasa, Naibu rais alisema kwamba maafisa wa DCI, wamekuwa wakitumia nyadhifa zao visivyo wakiwanyanyasa watu hasa wa nyadhifa za kisiasa.  

Alisema unyanyasaji huo umekuwa ukiwazuia maafisa hao kutekeleza majukumu yao ya kikatiba.  

“Nataka niwahakikishie tunafahamu unyanyasaji na vitisho kwa magavana vinavyofanywa na vyombo vya usalama,” alisema. 

Kulingana na Gachagua, DCI haina mamlaka ya kuingilia maswala ya mashirika ya serikali, isipokuwa ni suala la umuhimu mkubwa kwa umma, kwa hivyo maafisa hao wanafaa kujiepusha na kuzingira afisi za serikali za kaunti kwa lengo la kuwakamata viongozi. 

"Tumeambia DCI kurudi katika Barabara ya Kiambu na kusubiri uhalifu kuripotiwa huko. Hawana biashara katika afisi za serikali wakizunguka pande zote na kuweka mazingira ya sumu kwa utoaji wa Huduma," alisema. 

"Hatuwezi kuwa na wapelelezi katika ofisi za serikali kwa sababu wanatia hofu watumishi wa umma kufanya kazi." 

Gachagua vile vile alimsuta DCI kwa madai ya kutuma maafisa wa vyeo vya chini kuwakamata viongozi wa ngazi za juu waliochaguliwa, akibainisha kuwa hii inadunisha hadhi na mamlaka ya viongozi machoni mwa walio chini yao. 

“Mkuu wa asasi husika amwandikie barua gavana mwenyewe na asiwatume baadhi ya maofisa wa ngazi za chini kwenda kuongea na gavana kwa sababu hiyo si sawa na hayo ndiyo mambo tunayokwenda kuyafanya ili kurudishia heshima viongozi wetu,” alisema.