Joho asema kuwa kwa upinzani sio kifo, ataka Ruto kutekeleza ahadi zake

Joho alisema yuko imara katika upinzani na watakuwa na msimamo thabiti wa kuweka serikali katika darubini

Muhtasari

• Aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho amesema kwamba kuwa kwenye upinzani sio kitanzi. 

Aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho amesema kwamba kuwa kwenye upinzani sio kitanzi. 

Akizungumza mjini Mombasa katika hafla ya kuapishwa kwa Gavana mpya Abdulswamad Nassir, Joho alisema kuwa mbunge mmoja alimkejeli kwa kile alichokisema kwenye mkutano mmoja. 

Joho alimjibu kwamba kuwa kwa upinzani hakuna madhara, akiongeza kuwa hawezi kutishiwa na wanasiasa chekechea. 

“Kuna mwanachama wa UDA alinitumia video niliyoyasema wakati wa kampeni, nataka nikuambie kuwa kwa upinzani si hukumu ya kifo rafiki yangu. Mtu mpumbavu wa kutishia lakini sio mimi.Na nikamwambia kuwa yeye ni mdogo wangu na hawezi kuniambia chochote. Kuna watu wanaweza kutishiwa na watu hawawezi,'' Joho alisema.

Joho aliendelea kubainisha kuwa yuko imara katika upinzani na watakuwa na msimamo thabiti wa kuweka serikali katika darubini kila watakapokosa kutimiza ahadi walizotoa kwa Wakenya. 

"Tuko imara, serikali inapoingia ina majukumu, lazima tuiangalie na tuikosoe pale wanapokosea. Na leo nimefurahi kwa sababu bandari imerejea lakini tunataka kuona inafanya kazi," alisema Joho. 

"Jana niliwauliza watu wa bandarini kama wameanza agizo walilopewa na rais juzi, wakasema hawana taarifa za mawasiliano rasmi tunawaangalia kwa makini". 

Joho zaidi alimsifu mrithi wake Abdulswamad kwa ushindi wake, akielezea imani kwamba ataleta mageuzi yanayohitajika Mombasa. Aliongeza kuwa hataingilia masuala ya serikali iliyoko madarakani na kwamba mrithi wake atafanya kazi kwa uhuru bila shuruti. 

"Napitisha kitufe kwa kaka yangu Abdulswamaad, nina imani utayaendeleza tuliyoyafanya na kuyaleta mazuri zaidi ya tuliyoyafanya. Nakuombea kwa Mungu akupe hekima, uwezo na ujasiri wa kusimamia watu," alibainisha Joho.