Shirika la ndege la Kenya lateta vikali kukamatwa na kuzuiliwa kwa wafanyikazi wake DRC

"unasikitishwa na hatua hii inayolenga wafanyikazi wasio na hatia na tunachukulia kuwa ni unyanyasaji unaolenga biashara ya Kenya Airways,” Kilavuka alisema.

Muhtasari

• Taarifa hiyo ya malalamiko ilisema kwamba wafanyikazi hao wameendelea kuzuiliwa licha ya mahakama ya kijeshi kuamuru waachiliwe.

• KQ ilieleza ukweli kuhusiana na tukio hilo, na kusisitiza kuwa shehena hiyo haijakabidhiwa kwao na bado inafanyiwa kibali.

Ndege ya Kenya Airways
Image: MAKTABA

Shirika la ndege la Kenya limetoa taarifa yao, wiki moja baada ya wafanyikazi wake kukamatwa na kuzuiliwa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kisa hicho, kilichotokea Ijumaa, Aprili 19, kilizua wasiwasi kuhusu kiteondo hicho kwa wafanyakazi wa shirika hilo la ndege na kufuata taratibu zinazofaa.

Kukamatwa huko kulihusishwa na madai ya hitilafu katika hati maalum za shehena ya thamani iliyoratibiwa kusafirishwa kwa ndege ya KQ.

Hata hivyo, KQ imefafanua kuwa shehena husika haikukubaliwa kamwe au kuinuliwa kutokana na kutokamilika kwa nyaraka.

"Wakati wa kukamatwa kwao, simu zao zilinaswa na kukataliwa kuwafikia. Jumatano, Aprili 23, maafisa wa ubalozi wa Kenya na wafanyikazi wachache wa KQ waliruhusiwa kuwatembelea lakini kwa dakika chache tu," Mkurugenzi Mtendaji wa Kenya Airways Alan Kilavuka alisema katika taarifa kwenye ukurasa wao wa X.

Taarifa hiyo ya malalamiko ilisema kwamba wafanyikazi hao wameendelea kuzuiliwa licha ya mahakama ya kijeshi kuamuru waachiliwe.

KQ ilieleza ukweli kuhusiana na tukio hilo, na kusisitiza kuwa shehena hiyo haijakabidhiwa kwao na bado inafanyiwa kibali.

Juhudi za kuwasilisha hili kwa maafisa wa kijeshi hazikufaulu, na kusababisha kuzuiliwa kwa wafanyikazi katika kituo cha DEMIAP.

“Ukaguzi wetu wa utiifu wa ‘Tayari kwa Usafirishaji’ ni mkali, na kuhakikisha kwamba mizigo yote inakidhi mahitaji ya kisheria kabla ya kukubalika. Tunasikitishwa na hatua hii inayolenga wafanyikazi wasio na hatia na tunachukulia kuwa ni unyanyasaji unaolenga biashara ya Kenya Airways,” Kilavuka alisema.

Alisisitiza zaidi kwamba jukumu la uhifadhi wa hati na idhini ni la msafirishaji au mshirika wa usafirishaji, sio shirika la ndege.