Ghost Mulee azungumzia maisha yake; kulelewa na single mother, kudaiwa kutumia uchawi...

Mtangazaji huyo alitaja kuwa watu wana dhana potofu kwamba alikuwa akitumia uchawi (ndumba) wakati akiwa kocha wa Harambee Stars.

Muhtasari

•Kati ya mambo aliyozungumza kuhusu ni pamoja na kulelewa na mama asiye na mume, wakati wa aibu zaidi kazini, mipango ya Valentines, miongoni mwa wengine.

•Ghost alifichua kuwa alitiwa msukumo sana na marehemu mamake kwani aling’ang'ana kabisa kumlea yeye na ndugu zake wengi akiwa pekee yake.

Jacob Ghost Mulee
Image: RADIO JAMBO

Mtangazaji mashuhuri wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Jacob ‘Ghost’ Mulee amejibu baadhi ya maswali ya kibinafsi kumhusu.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Harambee Stars alifichua baadhi ya maelezo kuhusu maisha yake wakati wa mahojiano ya haraka na mwanahabari Samuel Maina.Kati ya mambo ambayo alizungumza kuhusu ni pamoja na kulelewa na mama asiye na mume, wakati wa aibu zaidi kazini, mipango ya Valentines, miongoni mwa wengine.

Ghost alifichua kuwa alitiwa msukumo sana na marehemu mama yake kwani alitia bidii sana na akang’angana kabisa kumlea yeye na ndugu zake wengi akiwa pekee yake.

"My inspiration ofcourse is my late mother, ndiye alikuwa ananitia msukumo sana kwa sababu alitulea tukiwa watoto wengine na yeye ni single mother," Ghost alisema.

Aliongeza, "Hiyo ni moja ya msukumo wangu mkubwa zaidi kwa dunia hii."

Kuhusu kipindi chake cha aibu zaidi kazini, mtangazaji huyo mahiri wa redio alibainisha kuwa kazi yake kwenye redio imekuwa laini kabisa na haijawahi kuwa na wakati wa aibu ambao anaweza kukumbuka.

“Kipindi cha aibu zaidi hewani, siwezi nikakumbuka. Sidhani kama nishawahi kupata any embarrassing moment,” alisema.

Ghost pia alitaja kuwa watu wana dhana potofu kwamba alikuwa akitumia uchawi wakati akiwa kocha wa timu ya taifa ya soka ya Kenya, madai ambayo alibainisha kuwa sio ya kweli.

"Maoni potofu kuhusu mimi ambayo watu wengi wanayo ni kwamba, nikiwa Harambee nilikuwa natumia ndumba (uganga)," alisema.

Huku akizungumzia mipango yake ya Siku ya Wapendanao, mtangazaji huyo mcheshi wa redio alibainisha kuwa anafurahia sana kwa kuwa siku hiyo kwani itakuwa ni ‘Jumatano ya Majivu’ kwa Wakatoliki.

“Hii Valentines ata nimefurahia sana kushukuru Baba Mtakatifu, kwa sababu hiyo ni siku yetu ya kuanza kufunga. Tunaanza kufunga hiyo siku, ni ash Wednesday,” alisema.

Pia alifichua kuwa kazi yake ya kwanza, alifanya kazi kama mfanyakazi wa kawaida ambapo angepata chini ya shilingi mia tano kwa wiki.

“Kazi yangu ya kwanza ilikuwa kibarua huko Kenya Airways, tulikuwa tunalipwa karibu 70 bob per day. Tulikuwa tunalipwa kila baada ya wiki mbili ama kila wiki. Kwa hiyo najua 70*7, ilikuwa napata karibu 490 kwa wiki,” Ghost alisema.

Aliongeza, “Wakati huo 70 ilikuwa pesa nyingi, unajua sio juzi. Ni 1989 huko.”

Jambo lingine ambalo mtangazaji huyo alifichua ni alama zake za sekondari ambapo alisema alifaulu vizuri sana.

“Nilipata alama nzuri juu nilihitimu kwenda High school. Nilipata alama nzuri kusema kweli, sikumbuki ni nini lakini nilipata alama nzuri lakini nilihitimu nikaingia form 5 na form 6,” alisema.

Kuhusu vile angekuwa kama asingekuwa mtangazaji wa Redio, alisema, “Kama nisingekuwa Mtangazaji wa Redio, ningekuwa KDF ama ningekuwa KWS. Ningekuwa mtu nashughulika na wanyama.