Uamuzi wa Martha Koome ulikuwa wa kishetani - Raila

Alipuuzilia mbali madai ya Jaji mkuu Martha Koome kwamba uamuzi wake ulichochea na mkono wa Mungu.

Muhtasari

• “Nina hofu kuwa huenda uamuzi wa Koome ukadhoofisha demokrasia ya upigaji kura nchini."

Raila Odinga
Raila Odinga
Image: Hisani

Kinara wa Upinzani Raila Odinga amekosia vikali mahakama ya upeo kwa kukubali kutumika kisiasa na kutoa maamuzi ya kishetani. 

Raila ambaye alikuwa alihutubikia mkutano wa wabunge wa muungano wa Azimio One Kenya siku ya Ijumaa alisema kwamba uamuzi uliyotolewa na Jaji mkuu Martha Koome kuhusiana na matokeo ya uchaguzi haukuwa wa kisheria bali ulikuwa wa kisiasa. 

Waziri huyo mkuu wa zamani alisema kwamba maneno yaliotumiwa na jaji mkuu wakati akitoa uamuzi wake yalikuwa ya kudhalilisha na ilikuwa wazi kwamba yalikuwa na kinyongo. 

Alisema lugha aliotumia Koome siyo lugha ya mahakama “...Miaka hii yote hata mawakili wenye uzoefu watakuambia hawajawahi kusikia matumizi ya maneno ya kudhalilisha kama hot air, wild goose.” 

Alipuuzilia mbali madai ya Jaji mkuu Martha Koome kwamba uamuzi wake ulichochea na mkono wa Mungu akisema kwamba kulingana na yeye uamuzi wa Koome ulitokana na nguvu za shetani. 

“Juzi Koome akiwa kwa mazishi alijipiga kifua akisema kwamba uamuzi wake ulikuwa kutokana na nguvu za Mungu, mimi nasema uamuzi wake ulitokana na nguvu za shetani,”Raila alisema. 

Kinara huyo wa ODM pia alionya kuwa serikali tayari imeanza mpango wa kuiteka nyara idara ya mahakama hatua ambayo alisema inalenga kurejesha taifa katika siku za giza. 

“Nina hofu kuwa huenda uamuzi wa Koome ukadhoofisha demokrasia ya upigaji kura nchini, jambo ambalo tumelipigania sana,” Raila aliongeza. 

Alitaka Jaji mkuu kuacha kuatishia watu wanaokosoa uamuzi uliotolewa na mahakama ya upeo kuhusiana na kesi ya uchaguzi wa urais. 

Raila alidai kuwa Rais William Ruto tayari ameanza kuhonga idara ya mahakama na siku zijazo idara hiyo itapoteza uhuru wake. 

Kiongozi wa upinzani aliwataka viongozi waliochaguliwa kwa muungano wa Azimio One Kenya kusalia pamoja wakiwa bungeni na kujiepusha na jitihada za kushawishiwa kujiunga na Muungano wa Kenya Kwanza. 

Alionya bunge dhidi ya kutumiwa na serikali kutishia maafisa wa idara mbali mbali ikiwemo idara ya polisi. Raila alimkashifu Naibu rais Rigathi Gachagua kwa kumlenga mkurugenzi wa DCI George Kinoti katika mashambulizi yake. 

Alisema kama kiongozi wa Azimio ataongoza jeshi lake kuhakiki kuwa idara ya mahakana inaokolewa pamoja na kufanyia mageuzi tume ya IEBC.