Raila akutana na Gachagua mjini Mombasa

Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi hao wawili kukutana tangu uchaguzi wa Agosti 9.

Muhtasari

• "Tuna heshima wazee wetu. Nilifurahi asubuhi ya leo kuwa na mazungumzo na mzee wetu Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga," Gachagua aliandika. 

Naibu Rais Rigathi Gachagua na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga.
Naibu Rais Rigathi Gachagua na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga.
Image: GACHAGUA/FACEBOOK

Naibu Rais Rigathi Gachagua na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga wamekutana mjini Mombasa. 

Wawili hao walikutana siku Ijumaa asubuhi ingawa maelezo ya mkutano wao bado ni finyu.  Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi hao wawili kukutana tangu uchaguzi wa Agosti 9. 

Katika ujumbe kwenye mtandao wa Facebook, Gachagua alifichua habari za mkutano wao katika Uwanja wa Ndege wa Moi chumba cha watu mashuhuri na kuweka picha wakiwa pamoja wakishauriana. 

"Tuna heshima wazee wetu. Nilifurahi asubuhi ya leo kuwa na mazungumzo na mzee wetu Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga," Gachagua aliandika. 

Raila alisemekana kuwa safari kwenda Machakos kwa Kundi la Wabunge wa Azimio naye Gachagua alikuwa akirejea Nairobi baada ya kufungua rasmi warsha ya kujitambulisha kwa Magavana. 

Raila alirejea nchini siku ya Alhamisi, baada ya kuwa nje kwa siku kadhaa. Alielekea Mombasa moja kwa moja kwa dhifa ya uapisho wa Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir katika hoteli ya Sarova Whitesands. 

Raila alikuwa ameenda kujivinjari pamoja na familia yake nchini Zanzibar kwa kile alichosema ni ‘kutafakari na kupona’ baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu matokeo ambayo alisema yalishtua familia yake. 

“Nimekuwa nje ya nchi; Nilikwenda kupata nafuu kisiwani Zanzibar. Nilimchukua mke wangu, watoto na wajukuu zangu pia ili kwenda kupona baada ya mshtuko walioupata kama familia,” alisema.