Martha Koome achapisha majina ya majaji watakaosikiza kesi za uchaguzi

Kati ya kesi 123 zilizowasilishwa, 12 ni za uchaguzi wa ugavana.

Muhtasari

• Katika Notisi ya Gazeti la tarehe 16 Septemba, Koome alibainisha maeneo ambapo kila hakimu atahudumu na kesi atakazoshughulikia.

Jaji Mkuu Martha Koome
Image: BBC

Jaji Mkuu Martha Koome amechapisha kwenye gazeti rasmi la serikali majaji na mahakimu watakaosikiliza kesi za kupinga uchaguzi kutokana na Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Katika Notisi ya Gazeti la tarehe 16 Septemba, Koome alibainisha maeneo ambapo kila hakimu atahudumu na kesi atakazoshughulikia.

“Kanuni za kesi za uchaguzi (Ubunge na kaunti) za mwaka 2017, kwa kutumia mamlaka yaliyotolewa na Kifungu cha 75 cha Sheria ya Uchaguzi, 2011 na Kanuni ya 6 (3), Jaji Mkuu anaagiza kwamba Malalamiko ya Uchaguzi ambayo maelezo yake yametolewa hapa chini yatasikilizwa katika Mahakama za Uchaguzi zinazojumuisha Majaji na Mahakimu walioorodheshwa na kukaa katika vituo vya Mahakama vilivyoonyeshwa kwenye jedwali hapa chini,” ilisema sehemu ya notisi hiyo.

Jaji Mkuu Martha Koome mnamo Machi 2022 alikuwa ameteua mahakimu maalum 119 kusikiliza na kuamua kesi za uchaguzi.

Uteuzi huo ulifanywa katika kaunti zote lakini baadhi ya vitengo vilivyogatuliwa vilipata mahakimu maalum zaidi kuliko vingine.

Nairobi ina idadi kubwa zaidi ya mahakimu maalum wakiwa saba huku Kiambu, Nakuru na Nyeri zikiwa na watano kila moja.

Mombasa na Kisumu zina wanne. Uasin Gishu, Migori, Murang'a, Machakos, Makueni, Siaya, Kisii, Kirinyaga, Kilifi, Embu, Bungoma na Kajiado watatu kila moja.

Malalamishi 123 hadi sasa yamewasilishwa katika vituo tofauti vya mahakama kuu nchini kote kupinga chaguzi mbalimbali.

Kati ya kesi 123 zilizowasilishwa, 12 ni za uchaguzi wa ugavana.

Kamati ya mahakama kuhusu uchaguzi inasema maombi hayo yaliwasilishwa kwenye jukwaa la kielektroniki kuanzia tarehe 14 Septemba.