logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Museveni ampandisha ngazi mwanawe Muhoozi baada ya jumbe tata kuhusu Kenya

Jenerali Muhoozi amepandishwa ngazi hadi cheo cha Jenerali Mkuu.

image
na Davis Ojiambo

Habari04 October 2022 - 12:52

Muhtasari


  • • Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda inasema kuwa serikali haifanyi sera za kigeni kwenye mitandao ya kijamii.
Jenerali Muhoozi Kainerugaba

Baada ya jumbe tata kuhusu Kenya mwanawe rais wa Uganda, Muhoozi Kainerugaba, amepandishwa ngazi katika mabadiliko ya hizi punde yaliotangazwa katika usimamizi wa majeshi ya nchi hiyo.

Kulingana na habari katika vyombo vya habari nchini humo Jenerali Muhoozi ambaye alikuwa mkuu wa jeshi la nchi kavu amepandishwa ngazi hadi cheo cha Jenerali Mkuu na nafasi yake kuchukuliwa na Kayanja Muhanga. 

Serikali ya Uganda awali ilikuwa imejibu mjadala wa mitandao ya kijamii ulioibuliwa na Muhoozi Kainerugaba kwenye msururu wa ujumbe wa Twitter ambapo alisema jeshi la Uganda linaweza kushambulia Kenya.

Kamanda huyo alisema kwamba itamchukua yeye na jeshi lake wiki mbili kuuteka mji mkuu wa Nairobi.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda ilisema kuwa serikali haifanyi sera za kigeni kwenye mitandao ya kijamii, na kwamba Uganda inathamini uhusiano mkubwa uliopo kati ya nchi hizo mbili na Kenya.

Inaongeza kuwa nchi hizo mbili zina historia ya pamoja, kuheshimiana kwa uhuru wa kila mmoja wao, kuaminiana na kutaka kujenga jumuiya yenye umoja ya Afrika mashariki.

Msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia Felix Kulayigye alisema Uganda ina uhusiano mwema na Kenya na hivyo jeshi la Uganda haliwezi kuivamia nchi hiyo jirani.

Miongoni mwa tweets zake ni kwamba alisikitishwa kwamba rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta aliondoka madarakani kwa sababu angeshinda uchaguzi mwingine kwa urahisi.

Lakini Jumanne asubuhi, Jenerali Kainerugaba alisema kuwa alizungumza na babake Rais Yoweri ambaye angetangaza mabadiliko, lakini haijabainika iwapo Jenerali huyo alikuwa anazungumzia mabadiliko katika jeshi.

Aliongeza kuwa dhamira yake na ya kizazi cha vijana ni kufanya kazi kuelekea shirikisho la Afrika mashariki, ambalo anatarajia kuliongoza jeshi. Serikali ya Kenya bado haijajibu rasmi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved