Taarifa kutoka Afrika Kusini zinasema kuwa nchi hiyo ina mpango wa kuhalalisha biashara ya ngono kama njia moja ya kupiga vita maambukizi ya janga la UKIMWI na pia kuzuia dhuluma za kingono dhidi ya wanawake.
Uuzaji na ununuzi wa huduma za ngono hautachukuliwa tena kama uhalifu chini ya sheria iliyopendekezwa na kuwasilishwa na wizara ya sheria. Kulingana na vikundi vya utetezi kuna zaidi ya wafanyabiashara wa ngono 150,000 nchini humo.
"Inatarajiwa kuwa kuhalalisha kutapunguza ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya wafanyabiashara ya ngono. Pia ingemaanisha upatikanaji bora wa huduma za afya na... kumudu ulinzi bora kwa wafanyabiashara wa ngono, mazingira bora ya kazi na kupunguza ubaguzi na unyanyapaa " Waziri wa Sheria Ronald Lamola alinukuliwa na jarida la CBS nchini humo Ijumaa wiki jana.
Katika bara la Afrika, Afrika Kusini ina moja ya idadi kubwa ya watu walio na Virusi vya UKIMWI na imekumbwa na ongezeko la wimbi la unyanyasaji dhidi ya wanawake kwa muda mrefu.
Katiba ya Afrika Kusini baada ya kipindi kirefu cha ubaguzi wa rangi ni miongoni mwa katiba huria zaidi duniani, ikiruhusu kuwepo kwa sheria zinazoendelea kuhusu uavyaji mimba na ndoa za jinsia moja, lakini biashara ya ngono kwa muda mrefu imesalia kuwa suala la mgawanyiko.
Mswada huo, ambao umechapishwa kwa maoni ya umma, unahusu tu kuharamisha biashara ya ngono na haudhibiti biashara ya ngono.