Kiongozi wa Azimio Raila Odinga sasa anasema kwamba atamshtaki Rais William Ruto kwa kumharibia jina.
Akizungumza mjini Nakuru siku ya Alhamisi, Raila alisema aliondolewa mashtaka ya uhaini, lakini Ruto ameendelea kuharibu jina lake.
Alisema mahakama haikupata ushahidi wowote kwamba alishiriki katika jaribio la 1982 la kupindua serikali ya Rais wa zamani Daniel Moi.
“Niliondolewa mashtaka ya uhaini baada ya mahakama kugundua kuwa hakuna ushahidi ulionihusisha na jaribio la mapinduzi ya 1982. Ruto ameharibu jina langu na nitaenda kumshtaki kwa kunichafuliwa jina,” alisema.
Alisema kuwa serikali ya wakati huo ilimzuilia katika Gereza la Kamiti Maximum kwa miezi sita alipokuwa akikabiliwa na mashtaka mahakamani, lakini akashinda kesi hiyo mwaka wa 1983.
Waziri Mkuu huyo wa zamani mnamo Alhamisi alipeleka kampeni zake za kupinga serikali hadi Nakuru.
Aliandamana na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa DAPK Eugene Wamalwa miongoni mwa wengine.